Zanzibar kuweka mkazo zao la mwani
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuweka mkazo kwenye sekta ya mwani ili kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuzipatia soko la uhakika.
Dk Mwinyi amesema hayo leo Agosti 21, Ikulu Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Tanzania,Christine Grau.
SOMA: Dk Mwinyi: Kiwanda cha mwani mageuzi makubwa kiuchumi
Amesema asilimia 99 ya wakulima wa zao la mwani Zanzibar ni wanawake, hivyo alimueleza balozi huyo kuona haja ya kuwaunga mkono wanawake hao na wakulima wa mwani nchini kwa kuwapatia mafunzo na vifaa vya kisasa ili wazalishe mwani wenye ubora utakaoendana sambamba na soko la uhakika.
View this post on Instagram
Dk Mwinyi alimueleza Balozi Grau kuwa Uchumi wa Buluu ni sera kuu ya uchumi wa Zanzibar hivyo amemueleza kuangalia fursa zinazopatikana na sera hiyo.
Kwa upande wake Balozi Christine Grau amesifu juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kuwa wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kushirikiana na jamii kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa jamii .