Z’bar yazindua hatifungani ya Kiislamu ya kwanza EAC

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imezindua hatifungani inayozingatia misingi ya sheria ya Kiislamu inayoitwa Zanzibar Sukuk.

Hatifungani hiyo ni ya kwanza kutolewa na serikali katika nchi zote za jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuzingatia misingi ya kisheria ya Kiislamu.

SMZ imesema wakati umefika wa kuifanya benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kuwa benki kubwa itakayosaidia wananchi na nchi bila kuuzwa kwa mtu yeyote. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amezindua hatifungani hiyo katika viwanja vya Ikulu Unguja jana.

Hatifungani hiyo itatumika kukusanya fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo Zanzibar. Akizungumza katika uzin[1]duzi huo, Dk Mwinyi alisema fedha zitakazopatikana zitatumika kuijenga Zanzibar na kutoa faida kwa wawekezaji.

“Hatifungani hii sio tu muhimu kwa nchi lakini pia, kwa faida ya kila mmoja kwani fedha zitakazopatikana zitatumika kuijenga nchi yetu na wawekezaji wote watapata faida ya halali inayokidhi sheria ya Kiislamu,” alisema.

Dk Mwinyi alisema utaratibu wa kibajeti hautoshelezi kutekeleza miradi kwa wakati hivyo serikali imebadili namna ya kutafuta rasilimali fedha kwa lengo la kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya kiuchumi. Dk Mwinyi alisema uwepo wa hatifungani ya Zanzibar Sukuk utaimarisha uchumu na kusaidia kuweka utulivu katika mifumo ya kifedha na kuhakikisha usalama wa fedha za wawekezaji pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mikakati imara ya kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaumarika. Dk Mwinyi ameziita taasisi za umma kuwekeza katika hatifungani hii akisema ni fursa kwa wananchi, vikundi, wafanyabiashara na sekta binafsi kuwekeza katika Zanzibar Sukuk.

Katika hatua nyingine, Dk Mwinyi alikemea viongozi wanaosambaza taarifa za uongo na upotoshaji kuhusu kuuzwa kwa Benki ya PBZ. “Kuna kiongozi wa siasa anasimama katika majukwaa akisema serikali hii inakusudia kuiuza Benki ya PBZ, nataka nimwambie kama anasema kwa kutojua tutamfahamisha lakini kama anasema kwa kupotosha basi sisi ni viongozi tutamuelimisha,” alisema.

Aliongeza: “Kila kinachofanya watu wakaleta maneno maneno naomba wananchi wawapuuze hawajui wanachofanya, kusema jukwaani kila mtu anaweza lakini elimu na weledi uwe navyo kwanza kabla hujaropoka”. Dk Mwinyi alisema uwekezaji unafanyika katika Benki ya PBZ kwa kutumia wawekezaji wa nje ambao wanalenga kuwezesha mitaji, teknolojia na kutumia nguvu kazi ya wawekezaji hao ili PBZ iweze kutoa mikopo mikubwa na si midogomidogo kama ilivyo sasa.

Hatifungani ya Zanzibar Sukuk inakusudia kukusanya trilioni 1.115 ikiwa na kiwango cha chini cha kuwekeza cha Sh milioni moja na faida ya uwekezaji, ikiwa ni asilimia 10.5 kwa mwaka. Faida hiyo itatolewa kwa awamu mbili ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia miaka saba na wawekezaji watapata faida ya uwekezaji na kuwaweze[1]sha kuwekeza tena faida watakayoipata wakitaka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button