Zijue sheria zitakazowatia hatiani wasambazaji picha chafu

DODOMA: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amewataka Watanzania kuungana katika kudhibiti vitendo viovu kwa kumtumia picha mnato au mjongeo zenye kuonesha viungo na mambo ya sirini mitandaoni yanayochangia mmomonyoko wa maadili.

Waziri Gwajima ameeleza hayo leo kwenye akaunti rasmi ya Instagram ya waziri huyo ambapo amesema atatumia video na picha hizo kama ushahidi dhidi ya ukiaukwaji wa sharia.

“Wahini wahini download video na picha za watu wanatikisa tikisa na kuonesha viungo na mambo ya sirini hadharani Ili tuwaoneshee vifungu vyao vya sheria vikoje,” amesisitiza kiongozi huyo.

Advertisement

Hata hivyo, ametahadharisha kuwa kuna wengine amesikia wameanza kufuta aibu zao online ‘mtandaoni’ kwa kasi kubwa.

“Wahi download, kisha piga screen shot na ukurasa mzima kabla hajaondoa. Tupate kianzio, maana maneno tumesema na kurudia rudia wamejifanya hawasikii lolote wala chochote na sheria hawajataka kuzisoma,” amefafanua Gwajima.

Amesema, wanaohusika na vitendo hivyo wanafanya mambo kinyume cha sharia, hivyo amewashangaa ni hivi hata hawakumbuki hata kuwauliza wanasheria wao ni lipi jema na lipi baya.

“Haiwezekani tukawa tunasema tu na wao wanafanya tu. Imetosha. Wahi wahi vielelezo. Wengine wameshaniletea kadhaa,” amesisitiza.

Hata hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) yenyewe haina kifungu kinachozungumzia moja kwa moja marufuku ya kuonesha video au picha za utupu kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, suala hili linashughulikiwa na sheria nyingine za nchi zinazodhibiti maudhui ya mtandaoni na kudumisha maadili ya jamii.

Sheria zinazohusika ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015. Sheria hii inakataza kusambaza maudhui yenye maudhui ya aibu, yanayokiuka maadili au kuhamasisha tabia zisizo za kimaadili kupitia mitandao.

Ibara ya 16 na 17 ya Sheria hii inazuia usambazaji wa picha za utupu au maudhui yasiyofaa mtandaoni, na mtu anayekiuka sheria hii anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010. Sheria hii, kupitia Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za Mwaka 2018 ‘Online Content Regulations’, inatoa mwongozo wa kudhibiti maudhui yasiyofaa, ikiwemo picha na video za utupu, kwenye mitandao ya kijamii. Inazuia waziwazi uoneshaji na usambazaji wa maudhui yoyote yanayokiuka maadili na mila za Kitanzania mtandaoni.

Sheria hizi zinatoa mamlaka kwa serikali kudhibiti aina ya maudhui yanayoruhusiwa kusambazwa mtandaoni na kuhakikisha kuwa yanazingatia maadili na usalama wa jamii.