‘Zingatieni wajibu na maadili ya kazi zenu’

WATENDAJI na watumishi wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wametakiwa kutimiza wajibu na maadili ya kazi pindi wanapokuwa katika majukumu yao.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete katika kikao kazi cha kutoa mafunzo kwa watumishi, kilichoongozwa na Katibu huyo kilichofanyika eneo la Shule ya Msingi Bulamata, Kata ya Bulamata Tarafa ya Kabungu.

Mwashitete amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapitisha watumishi kwenye kanuni, taratibu na sheria mbalimbali za utumishi wa umma ili waweze kutimiza wajibu wao.

Ofisa Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Andrew Chiduo, akizungumza kwenye mafunzo hayo. (Picha zote na Swaum Katambo.)

Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha watumishi wa umma kwamba muda mwingi wautumie kuwahudumia wananchi pamoja na wadau mbalimbali.

Pia amesema viongozi wanaohusika kuhudumia wananchi wafike maeneo wanayotakiwa badala ya kusubiri kufuatwa ofisini.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Andrew Chiduo amesema lengo la kuwafuata watendaji na watumishi hao katika tarafa hiyo ni kuwakumbusha haki na wajibu wao katika majukumu yao, huku wakitarajia ufanisi zaidi katika kazi.

Nao baadhi ya watumishi mara baada ya kupata mafunzo hayo kwa nyakati tofauti waliahidi kuleta mabadiliko chanya katika majukumu yao.

“Tumekumbushwa mambo mengi ambayo mengine tuliyasahau, tumekumbushwa kudai haki zetu za msingi baada Ofisa Utumishi kutukumbusha haki na wajibu ambao inatakiwa tupate na tufanye, ili tupate haki zetu,” amesema Justin Erasto, Ofisa Mtendaji Kata ya Bulamata

Habari Zifananazo

Back to top button