Zitto, Lissu wamlilia Sarungi

KIONGOZI mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto amesema kiongozi mstaafu wa serikali, Profesa Philemon Sarungi alifanya kazi kwa weledi na alikuwa hazina kwa nchi.
Zitto alisema hayo nyumbani kwa marehemu juzi na kwamba kiongozi huyo ameacha alama ya kujituma na kujitoa.
“Taifa limepoteza hazina, limepoteza mwanataaluma mkubwa kama daktari wa mifupa lakini pia limepoteza waziri ambaye amefanya kazi kwa uadilifu mkubwa sana kwa muda mrefu,” alisema.
Aliongeza: “Alikuwa kiongozi anayejitoa, ile hali ya kujituma na kujitoa. Mnakumbuka wakati mzee Sarungi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani inatokea ajali yeye anakuwa mstari wa mbele kwenda kutibu majeruhi. Alikuwa kiongozi anayejitoa na sio kung’ang’ania nafasi yake.
Zitto alisema Profesa Sarungi ana mchango mkubwa katika maisha yake ya uongozi kwa kuwa alimlea wakiwa bungeni na alimfundisha mambo mbalimbali.
“Alikuwa mmoja wa wazee watatu waliokuwa wananilea katika shughuli za kibunge na ndani ya Bunge. Unajua Wajaluo na Waha ni watani, alikuwa ananitania, ananipeleka kantini tunakaa tunakunywa kahawa ananieleza umehutubia hivi, umekasirika hutakiwi kuongea hivyo unatakiwa kuongea hivi kwa hiyo alikuwa mtu ambaye ananifunda namna gani ya kukaa bungeni,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, hata profesa Sarungi alipomaliza muda wake uongozi aliendelea kuwa mshauri wake katika uongozi na alikuwa na uwezo wa kumpigia simu wakati wowote.
Alisema Profesa Sarungi alianza safari ya uongozi katika udiwani, baadaye akawa Mbunge wa Rorya, Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na waziri katika wizara tofauti.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu alisema profesa Sarungi aliitumikia nchi kwa heshima.
“Profesa Philemon Sarungi alikuwa ni mmoja wa wazee wetu wazee wa nchi yetu, watu ambao wameitumikia nchi hii kwa muda mrefu kwa heshima kubwa, wamefanya kazi ya kujenga nchi, wakakamilisha kazi yao wakapumzika,” alisema Lissu nyumbani kwa marehemu.
“Sikuwahi kupata bahati ya kufanya kazi moja kwa moja na Profesa Sarungi ila ninafahamu…kwa miaka yote ambayo ametumika nchi hii amefanya kazi bila mawaa kabisa,” alisema Lissu.
Imeandikwa na Shakila Mtambo na Eva Sindika.



