Aipongeza serikali kuimarisha mauzo ya kahawa nje ya nchi

KAGERA: Mwekezaji wa kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la kahawa mkoani Kagera, Amiri Hamza, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuboresha diplomasia ya biashara nje ya nchi na kufungua milango kwa wafanyabiashara wa kahawa kuuza bidhaa zao kimataifa bila vikwazo.

Akizungumza mbele ya wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Hamza ambaye anamiliki kiwanda cha kuchakata na kukoboa kahawa mkoani Kagera, amesema tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, mazingira ya biashara ya kimataifa yameimarika kwa kiasi kikubwa.

Amesema wafanyabiashara wa kahawa sasa wanafanya biashara katika masoko mbalimbali duniani kwa urahisi huku ofisi za ubalozi zikitoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania.

Hamza amesema tangu mwaka 2023 kumekuwa na urahisi wa kufungua ofisi na matawi ya kuitangaza kahawa ya Tanzania nje ya nchi, jambo ambalo limeendelea kuitangaza Tanzania pamoja na ubora wa kahawa yake duniani.

“Nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wangu Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ameifungua nchi kwa vitendo. Mimi kama mfanyabiashara napeleka kahawa yangu katika karibu nchi 57 bila vikwazo. Hakuna ubalozi ambao haufungui mlango. Kila ofisi iko wazi, hii ni hatua kubwa sana. Kahawa yangu inaitwa AMIMZA na imeandikwa inazalishwa Bukoba Tanzania, hakuna vikwazo,” amesema Hamza.

Aidha, amesema kiwanda chake kilikumbwa na changamoto ya kuungua kwa moto mwaka 2024 na kusababisha uharibifu wa miundombinu, lakini kwa sasa anaendelea na juhudi za kujenga upya kiwanda hicho.

Amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani 18,000 za kahawa na kuiomba serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani kwa kuwapatia mitaji ya uhakika ili waweze kushindana katika soko la dunia.

Hamza pia ameishukuru serikali kwa kuweka uwazi katika mfumo wa bei ya kahawa na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kununua kahawa kulingana na uwezo wao wa kifedha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Profesa Aurelia Kamuzora, amempongeza mwekezaji huyo kwa uwekezaji wake mkubwa katika kuongeza thamani ya kahawa na kuahidi kuyafikisha maombi na pongezi zake kwa mamlaka husika.

Amesema serikali inaendelea kushughulikia maombi ya wadau wanaohitaji kusaidiwa mitaji kupitia mifumo mbalimbali ya uwekezaji wa kiuchumi ili kuwawezesha kufanya biashara kwa ufanisi zaidi.

Wajumbe wa bodi hiyo pia wameeleza kuvutiwa na kiwango cha uwekezaji pamoja na miundombinu ya kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1994 na ambacho sasa kina zaidi ya miaka 30 ya shughuli za uzalishaji.

Licha ya changamoto ya kuungua kwa moto mwaka 2024, mwekezaji huyo anaendelea na hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi mpya wa kiwanda hicho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button