128 wapata huduma ya puto kupunguza uzito

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili Mloganzila hadi sasa imetoa huduma ya kupunguza uzito kwa watu 128 wenye uzito uliopitiliza kwa kutumia puto maalum (intragastic balloon).

Huduma hiyo pamoja na kupunguza uzito imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuwawezesha wateja hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi tofauti na ilivyokuwa awali. 

Kaimu Mkuu wa Idara ya Upasuaji MNH-Mloganzila Dk Erick Muhumba amesema kati ya watu hao 128 waliofanyiwa huduma hiyo wanawake wanne  wamefanikiwa kupata ujauzito ambapo mmoja wao alikaa zaidi ya miaka sita bila kupata ujauzito kutokana na tatizo la uzito uliopitiliza.

 

Amesema zaidi ya watu 12 wameondolewa puto hilo kutokana na uzito wao kupungua na wachache wameondolewa kutokana na maudhi madogo madogo waliyoyapata baada ya  kuwekewa puto hilo, hivyo kupelekea kuliondoa.

“Wapo baadhi ya wateja wetu takribani wanne tuliwawekea puto lakini tumelazimika kuliondoa kutokana na maudhi madogo madogo ikiwemo kutapika, lakini wengi wao huduma hii imekuwa rafiki na yenye mafanikio makubwa na wapo ambao wametoa baada ya uzito kupungua,” amesema Dk Muhumba

Amesema, wapo ambao wameongeza maji au kupunguza maji kwenye puto kulingana na mahitaji ya wateja, ametoa mfano kuwa miongoni mwa  waliongezewa maji kwenye puto kwa lengo la kuendelea kupunguza uzito ni msanii na balozi wa puto Mloganzila  Peter Msechu ambae atalazimika kukaa na puto hilo kwa mwaka mzima. 

Kwa upande wake msanii na balozi wa puto  Peter Msechu amesema kwa kipindi cha miezi sita amepunguza takribani kilo 17 kutoka 144 alizokuwa nazo awali na ameona umuhimu wa kuongeza maji kwenye puto kutokana na kuwa na kasi ndogo ya uzito kupungua.

Msechu ameongeza kuwa tangu awekewe puto ameweza kufanya majukumu yake kwa muda mrefu bila kuchoka, pia amebainisha kuwa uzito wake haujapungua kwa kasi kama alivyotarajia kutokana na kutofanya mazoezi kama alivyoshauriwa na wataalamu hali iliyotokana na ratiba yake kusongwa na majukumu mengi ya kitaifa.

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button