Twiga Cement yasaidia waathirika mafuriko Rwanda

KAMPUNI ya Saruji Tanzania Portland Cement ijulikanayo kwa jina la Twiga Cement imekabidhi tani 64 sawa na mifuko 1,280 ya saruji kusaidia waathirika wa mafuriko yaliyotokana na mvua nchini Rwanda.

Msaada huo ulikabidhiwa kwa Wizara yenye Dhamana ya Menejimenti ya Dharura (MINEMA) ya nchini humo ikiwa ni mchango wake wa kusaidia kurejesha na kujenga nyumba za waathirika wa maafa yaliyotokea katika mikoa ya Kaskazini na Kusini hivi karibuni.

Takribani nyumba 5,963 ziliharibika na kuacha watu 20,326 bila makazi kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwezi huu.

Advertisement

Akizungumza na HabariLEO Afrika Mashariki jana, Ofisa Mauzo wa Twiga Cement, Yusuph Kajela alisema wametoa msaada wa tani 64 za saruji kwa wananchi wa Rwanda kama msaada kwa wananchi wake walioathirika kwa kuwa ni miongoni mwa wateja wao wakubwa.

“Tumetoa msaada huu Rwanda kutokana na kuwa ni wateja wakubwa wa bidhaa zetu kuanzia kwa serikali hutumia bidhaa yetu kufanya ujenzi wa miradi mbalimbali na hata wananchi wake ni wateja wetu wakubwa,” alisema na kuongeza kuwa, wana soko kubwa la saruji nchini humo.

Mwakilishi wa kampuni hiyo, Augustin Mukama alikabidhi msaada huo kwa Katibu Mkuu wa Minema, Philippe Habinshuti.

Habinshuti alishukuru akisema: “Rwanda ni mshirika mkubwa wa Twiga Cement. Mbali na misaada ya aina mbalimbali inayotolewa kwa waathiriwa hivi sasa, misaada pia inahitajika kujenga upya nyumba na miundombinu itakayowawezesha kurejea katika maisha ya kawaida.”

Alisema kuwa kutoa vifaa vya ujenzi kwa watu walioathiriwa na maafa kupitia Wizara ya Usimamizi wa Dharura ni kielelezo cha huruma kwa watu walioathirika na serikali ya Rwanda kwa ujumla.

Msaada huo unatajwa kutolewa wakati mwafaka ikizingatiwa kwamba, Minema kwa kushirikiana na mashirika mengine ya serikali na washirika, inatarajiwa kujenga nyumba mpya katika maeneo salama kwa ajili ya waathirika walio katika mazingira magumu ambao nyumba zao ziliharibiwa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *