KAGERA: NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema serikali iko mbioni kufunga mitambo ya kamera za uchunguzi 6500 kwa kuanzia na majiji makuu manne ili kupunguza uharibifu na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini, Daniel Sillo akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Kagera alipokutana na Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hiyo ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA.
Amesema kuwa, Kamera hizo zitafungwa katika maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile maeneo ya masoko, viwandani na kwenye makampuni katika majiji makuu manne ikiwemo Arusha, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.
”Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha uongozi wake tunajivunia mengi kwani ameimarisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwasababu Jeshi la Polisi linaenda kwenye mradi mpya unaoitwa majiji salama utakaowezesha kufunga mitambo ya kamera za kisasa 6500 kama ilivyoelezwa kwenye Bajeti ya Fedha ya Jeshi la Polisi 2024/25 ya kuhakikisha haya majiji manne yako salama ikiwa ni awamu ya kwanza ”amesema Sillo
Katika hatua nyingine amekemea na kuelekeza Jeshi la Polisi nchini kusimamia suala la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji huku akiitaka jamii pia kubadilika na kurudi kwenye maadili ya kitanzania kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao kwa kuwafichua wahalifu wa aina hiyo.
“Ndugu zangu watanzania hakuna utajiri au mali zinazopatikana kwa njia ya kufanya ukatili au mauaji hivyo niwasihi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ambazo hazivunji sheria na taratibu za nchi kwani utajiri wa halali na wa amani unapatikana kwa kufanya kazi tu nasi vinginevyo” amesema Sillo
Katika Mkutano huo Sillo amezielekeza Idara za Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) nchini kushirikiana kuhakikisha vitambulisho hivyo vinatolewa kwa watanzania halali na kwa usahihi kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi bila kushinikizwa kutumika na wanasiasa ambao hawana nia nzuri.
SOMA: Polisi yadaka wezi wa magari, bajaji
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Brasius Chatanda kwa niaba ya viongozi wote waliohudhuria mkutano huo kutoka Idara mbalimbali amemuahidi Naibu Waziri Sillo kuwa, maelekezo na miongozo yote wameipokea kwa ajili ya utekelezaji .