640 waacha dawa za kulevya, waanza tiba ya methadoni

JUMLA ya watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na kuacha 640 wamesajiliwa na kupata huduma ya ushauri nasaha na tiba ya methadoni kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi.

Hayo yalisemwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Joyce Shoo wakati akisoma taarifa ya juhudi zinazochukuliwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Abdalah Shaib Kaim, alipotembelea kituo cha Organization of Youth Against Risk Behaviors (OYARB) kilichopo wilayani Kibaha.

Shoo alisema kati ya waraibu hao, wanaume ni 637 na wanawake watatu ambapo halmashauri imeendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya katika vituo vya kutolea huduma za afya, vyombo vya habari na mikusanyiko.

“Waraibu waliokuwa kwenye matibabu ni 431 wanaume wakiwa 428 na wanawake watatu ambao wanatumia matumizi salama ya tiba ya methadoni na walioacha matibabu ni 37,” alisema Shoo.

Aidha, dawa za kulevya zilizokamatwa bangi kilo 39 na gramu 569.2, heroin gramu 1.5 na kesi 87 zinaendelea kwenye hatua mbalimbali.

Kiongozi huyo wa mbio za mwenge Kitaifa, Kaim, alisema jitihada lazima zifanyike kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya.

Kaim alisema dawa za kulevya ni changamoto hasa kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa na serikali inachukua hatua mbalimbali kukabili matumizi ya dawa hizo.

Habari Zifananazo

Back to top button