TASAF yakamilisha ujenzi Kituo cha Afya Upenja

UNGUJA, Zanzibar: MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umekamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Upenja katika Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kazkazini Unguja, visiwani Zanzibar chenye thamani ya Sh milioni 342, kitakachoboreshwa upatikanaji wa huduma za afya muda wote kwa wakazi wa Upenja na shehia za karibu.

Kituo hicho kimezinduliwa rasmi leo Desemba 22 na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rahma Kassim Ali katika shamrashamra za kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kuzindua kituo hicho, Rahma Kassim Ali, ameipongeza TASAF kwa juhudi kubwa inazofanya katika kuboresha maisha ya wanufaika wa mpango na jamii kwa ujumla kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Amesema, TASAF imekuwa na mchango mkubwa katika kuinua hali za maisha na kipato kwa jamii nzima kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, na kuwasihi wananchi wa Shehia ya Upenja kutunza miundombinu uliyojengwa  ili idumu kwa muda mrefu kwa manufaa  ya wananchi wengi.

“Tunaishukuru na kuipongeza TASAF kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo huu wa kituo cha Afya Upenja, Kituo huki ni muhimu  sana kwani kitasaidia upatikanaji wa huduma zote muhimu za afya kama vile upasuaji, huduma za kinywa na meno,  Mama na Mtoto, huduma ya wajonjwa wa nje na huduma ya mionzi,” amesema.

SOMA: Mafanikio ya Tasaf yawakuna wafadhili

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa TASAF, Japeht Boaz amesema jumla ya Sh bilioni 15.18 zimetumika katika utekelezaji wa miradi ya mbalimbali visiwani Zanzibar.

Kati ya hizo, zaidi ya Sh bilioni 1.9 zilitumika katika kununua vifaa vya utekelezaji na Sh bilioni 13 kilitumika kulipa ujira kwa kaya za walengwa zaidi ya 35,000.

“Miradi iliyotekelezwa ni katika sekta ya afya,vmaji elimu mazingira misitu, barabara, uvuvi, kilimo umwagilaiji na muindombinu,” amesema.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha Pili, TASAF imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya elimu, afya na maji, ambayo imegharimu zaidi ya Shlingi bilioni 3.1.

“Kwa mwaka huu 2024, miradi mitatu yenye thamani ya shilingi milioni 750 imetekelezwa na kukamilika kwa upande wa Unguja katika shehia za Bambi, Kizimkazi dimbani na Upenja, Miradi mingine inaendelea kutekelezwa katika shehia za Donge, Uzi na Kizimkazi dimbani kwa jumla ya Sh milioni 306.6,” ameongeza.

Kukamilika kwa miradi hii, kutaongeza wigo wa upatikanaji wa huduma muhimu katika maeneo husika hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kuichumi na hatimaye kuendelea kutokomeza umaskini wa kaya.

Habari Zifananazo

Back to top button