DAR-ES-SALAAM: MKURUGENZI wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Abdalla Kilima, amewashauri Watanzania wanaofanya kazi nchini Oman kufuata mikataba ya kazi na sheria za kazi zinazohusiana ili kuepuka matatizo wanayoweza kukutana nayo wakiwa nchini humo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dailynews Digital, Balozi Kilima amesema kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kufuatilia changamoto wanazopata wafanyakazi wanaoenda kufanya kazi Oman, lakini akasisitiza kuwa kila mfanyakazi anapaswa kuzingatia mikataba yao ya kazi ili kujiepusha na matatizo yoyote yanayoweza kujitokeza.
“Siku zote haki hailetwi kwenye sahani kama sambusa. Unatakiwa kufuatilia haki yako ili uweze kulinda maslahi yako,” alisema Balozi Kilima.
Aliongeza kwa kusema, “Serikali tumetimiza wajibu wetu, na wewe na muajiri wako pia mna wajibu wa kutimiza.”
Wafanyakazi kutoka Tanzania wanaoenda kufanya kazi Oman wameshuhudia changamoto mbalimbali, ikiwemo kupokonywa hati zao za kusafiria mara tu wanapofika nchini humo.Hali hii inawafanya washindwe kupata msaada wanapokutana na matatizo.
“Mabosi wetu wanatutwaa hati za kusafiria na mara tunapokuwa na matatizo hatuwezi kufanya lolote,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa Kitanzania ambaye anafanya kazi Oman.
“Mara nyingi tunapokuwa na shida tunakimbilia ubalozini, lakini hatupati msaada wa kutosha.”
Akizungumzia suala hili, Balozi Kilima alisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hati ya kusafiria ni mali ya raia na serikali, na si mali ya muajiri.
“Hati ya kusafiria ni haki ya raia, sio ya muajiri. Kama huwezi kuihifadhi, unaweza kumkabidhi mwajiri wako, yeye ndiye anayetambulika na mamlaka za serikali,” alisema Balozi Kilima.
Pia alieleza kuwa kwa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nchini Oman, Serikali imeweka taratibu maalum kupitia Ofisi za Wakala wa Huduma za Ajira, TAESA kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kwa lengo la kukagua taarifa za ajira na safari zao. Huu ni mpango unaolenga kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wao wa kisheria.
Balozi Kilima aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira kwa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi Oman kwa kutoa mafunzo ya kazi wanazopaswa kufanya ili waweze kufahamu vyema taratibu na majukumu yao, hata kama ni kazi za nyumbani.
“Tumeingia mashirikiano na wadau mbalimbali kutoa mafunzo kwa kazi hizi ndogo ili kuwasaidia wafanyakazi wetu kufahamu majukumu yao,” alisema.
Tangu mwaka 2011, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia makubaliano ya kisheria na mataifa ya Mashariki ya Kati, ikiwemo Saudi Arabia, Oman na nchi za Falme za Kiarabu, kupeleka raia wake kufanya kazi katika nchi hizo.
TAZAMA: FAHAMU TARATIBU ZA AJIRA OMAN