Nchimbi ahimiza mambo 3 ushirikiano vyuo, waajiri

MAKAMU wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ameagiza mambo matatu ili kuhakikisha mpango wa ushirikiano kati ya vyuo na viwanda unatekelezwa kwa tija.

Dk Nchimbi alitoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliofanyika Dar es Salaam.

Alisema ni muhimu kwa sekta binafsi kushirikiana na vyuo kuwekeza katika tafiti hususani za sayansi na teknolojia.

Dk Nchimbi alihimiza ubunifu katika ufundishaji na ujifunzaji na kwamba kupitia mpango huo sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

Alisisitiza mafunzo kwa vitendo na akasema ushiriki wa waajiri na wenye viwanda katika utekelezaji wa mpango huo ni muhimu hususani katika uandaaji na mapitio ya mitaala, fursa za mafunzo kwa vitendo, uanagenzi na mafunzo kazini, ushiriki wa wataalamu viwandani katika ufundishaji, tathmini ya wanafunzi na uthibitishaji wa ujuzi na uimarishaji wa miundombinu ya mafunzo.

“Ushirikiano huo utawezesha sekta binafsi kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na mafunzo kazini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na waajiriwa wa fani mbalimbali,” alisema Dk Nchimbi.

Alitoa mwito kwa taasisi za elimu na sekta binafsi nchini kuzingatia maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa mpango huo.

Vile vile alitaka vyuo na sekta binafsi vishirikiane kubaini ujuzi muhimu unaohitajika sasa na siku zijazo hususani katika fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu ili kuwezesha vijana wetu kushindana na kupata nafasi katika soko la ajira hapa nchini na kimataifa,” alisema Dk Nchimbi.

Alisema mpango huo unalenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya utoaji wa elimu na utendaji kazi ilikulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele ikiwemo nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na viwanda vya kuongeza thamani.

Nchimbi alisema mpango huo unaweka msingi wa kujenga kizazi cha wahitimu wenye uwezo wa kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Alisema mpango huo utatekelezwa sambamba na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 pamoja na ajenda ya mageuzi ya elimu ya Zanzibar,” alisema.

Dk Nchimbi alisema serikali imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri.

Alisema dhamira hiyo inatokana na asilimia 34.5 ya Watanzania kuwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 wanaohitaji kuandaliwa kwa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la kitaifa na kimataifa.

Dk Nchimbi alisema kwa sasa zaidi ya wanafunzi milioni 2.1 wapo katika taasisi za elimu ya juu, ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button