Bil 5.3/- zawezesha wanawake Moro

MOROGORO: WANAWAKE 8,248 wa Mkoa wa Morogoro wamepata mipoko yenye thamani ya Sh bilioni 5.3 kupitia vikundi vyao kwa ajili ya kuwainua kiuchumi katika kipindi cha mwaka 2025 .

Mwenyekiti wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Morogoro, Sharifa Bofu, amesema hayo kupitia risala ya wanawake wa mkoa huo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika, kijiji cha Fulwe, kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro.

Sharifa amesema lengo la mikopo hiyo ni kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Katika hilo pia, ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia halmashauri zake inaendelea na uhamasishaji wananchi kujisajili kwenye mfumo wa Wafanyabiashara wadogo  ili kupatiwa mikopo inayotolewa Serikali yenye riba nafuu kupitia Benki ya NMB.

Katika hatua nyingine amesema hadi sasa majukwaa 775 ya uwezeshaji wanawake kiuchumi  kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya mkoa yameundwa kwa ajili ya kusimamia na kuratibu masuala mbalimbali ya wanawake .

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Lucy Kombani ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii amesema kumekuwa na tatizo la watoto kukatisha elimu licha ya Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Amesema serikali imekuwa ikihamasisha uandikishaji watoto darasa la kwanza na wanaoufauli elimu ya msingi kuendelea na sekondari bado kumekuwa na wimbi watoto kutomaliza elimu hususani ya  msingi.

“Wanafunzi wanaandikishwa darasa la kwanza wengi, na hawamalizi wote darasa la saba ,tunapoekelea kutekeleza dira ya Taifa 2050 elimu ni kipaumbele kikubwa ,  wazazi uwajibike kuwasimamia watoto wetu kielimu,” amesema  Kombani.

Mbunge huyo pia amesema kumekuwa na tatizo la ukatili wa kijinsia kwa  watoto na kwa kiwango fulani linachangiwa  na baadhi ya wazazi kufumbia macho  matendo hayoyanapotokea  kushindwa kutoa ushirikiano  kwa vyombo vya Serikali.

Kombani amesema kitendo hicho kinachangia  hata  yake matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yanapofikishwa vituo vya Polisi  kushindwa kuendelea Mahakamani kwa ukosefu wa ushahidi.

“Baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuelewana na waharifu wa matendo ya ukatili kwa watoto wao na hivyo kumweka mtoto kwenye matatizo ya maisha yake  na kumuathiri mtoto,”amesema Kombani.

Mbali na hayo amewataka  wanawake  hususani wazazi kusimama imara na watoto wao kuwapatia elimu na kuwaendeleza kwa kwa vile huo ndiyo msingi wa  maendeleo ya baadaye yanayotarajiwa na taifa letu kupitia Dira ya Taifa 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button