Kilimanjaro mwenyeji ya Siku ya Mkunga Duniani

KILIMANJARO: Mkoa wa Kilimanjaro unatarajiwa kuwa kitovu cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mkunga Duniani (IDM) mwaka 2026, ambapo Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kushirikiana na wadau wa afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana (RNMNCAH), kimeandaa matukio mbalimbali yatakayofanyika kuanzia Mei 2 hadi 5, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari Rais wa TAMA, Dk. Beatrice Mwilike amesema maadhimisho hayo yatapambwa na shughuli za uhamasishaji ikiwemo Mbio za Mkunga (Mkunga Half Marathon), maonyesho ya afya kwa jamii, utoaji wa huduma za afya pamoja na mafunzo maalum kwa wakunga.

“Lengo kuu likiwa ni kuonesha mchango mkubwa wa wakunga katika kuokoa maisha ya kina mama na watoto wachanga.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “dunia Inahitaji wakunga milioni 1 zaidi” ikiwa ni wito wa kimataifa wa kuongeza idadi ya wakunga na kuboresha huduma za afya ya uzazi.

Takwimu zinaonesha kuwa barani Afrika pekee kuna upungufu wa takribani wakunga 460,000, hali inayoweka maisha ya maelfu ya kina mama na watoto wachanga hatarini kila mwaka.

Mbali na upungufu huo, vituo vingi vya afya vinakumbwa na changamoto za mazingira yasiyo rafiki kwa utoaji huduma, ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama, vyoo bora pamoja na miundombinu duni ya usafi binafsi. Hali hii huathiri usalama wa mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Rais wa TAMA, Dk. Beatrice Mwilike, alisema upungufu wa wakunga haupaswi kuonekana kama takwimu tu bali ni suala la maisha ya watu.

“Upungufu wa wakunga si takwimu tu ni maisha ya kina mama na watoto yaliyo hatarini kila siku. Tunahitaji uwekezaji wa haraka, mafunzo zaidi na mazingira bora ya kazi kwa wakunga ili kuhakikisha hakuna mama au mtoto anayepoteza maisha wakati wa kujifungua,” amesema Dk. Mwilike.

Ameongeza kuwa wakunga ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uzazi salama, hivyo jamii, serikali na wadau wanapaswa kushirikiana kuimarisha taaluma hiyo.

Maadhimisho hayo pia yanalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa wakunga, kutoa mafunzo ya kitaaluma ili kuongeza ujuzi, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na sera madhubuti zitakazoboreshwa mazingira ya kazi kwa wakunga.

Aidha, TAMA imeweka lengo la kukusanya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya uzazi nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kwa ujumla, ujumbe mkuu wa maadhimisho haya ni kwamba kumwezesha mkunga ni kuokoa maishana kila mmoja ana nafasi ya kuchangia, iwe kama mdhamini, mshirika au mhamasishaji.

Wito umetolewa kwa jamii kushiriki kikamilifu na kuchangia juhudi hizi, kwa lengo la kuhakikisha kila mama na mtoto wanapata huduma salama na bora wakati wa kujifungua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button