Wanasheria EWURA wanolewa utatuzi migogoro

TANGA: Wanasheria wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) wanapatiwa mafunzo maalumu ya usuluhishi yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa lengo la kuwajengea uwezo, kuwapatia mbinu na maarifa ya kushughulikia migogoro na malalamiko ya wateja yanayowasilishwa katika mamlaka hiyo ikiwa ni njia mbadala ya utatuzi wa migogoro.
Mafunzo hayo ya wiki moja yameanza leo April 20, 2026 Chuoni Lushoto na yamefunguliwa na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA, Dk. Patricia Kisinda kwa niaba ya Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Paul F. Kihwelo.

Akizungumza wakati wa ufunguz, Dk. Kisinda amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea washiriki uwezo, maarifa na mbinu za kutatua migogoro na malalamiko kwa njia mbadala za utatuzi wa migogoro, hususani usuluhishi ili kupunguza utegemezi wa mashauri Mahakamani ambayo mara nyingi huchukua muda mrefu na kuathiri shughuli za kiuchumi.
Dk Kisinda amebainisha kuwa IJA ina jukumu la msingi la kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya haki kupitia mafunzo endelevu yanayoendana na mahitaji ya sasa ya mfumo wa haki.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa EWURA, Toni Mbilinyi, amesema kuwa wamehudhuria mafunzo hayo kwa kuwa EWURA hupokea na kushughulikia malalamiko ya wateja wa huduma, ambapo hatua ya mwanzo baada ya kuyapokea huwa ni usuluhishi.
Ameongeza kuwa kutokana na usuluhishi kuwa hatua ya kwanza katika utatuzi wa malalamiko ya wateja, wameona ni bora kwa watumishi wanaosikiliza malalamiko kuwa na weledi mpana wa mbinu za usuluhishi ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao.
Bi. Toni ameongeza : “Mafunzo haya yatawajengea uwezo na kuwapatia mbinu bora za utatuzi wa migogoro, jambo litakaloongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi”.

Kwa mujibu wa majukumu yake kisheria, EWURA ina wajibu wa kushughulikia malalamiko na migogoro kati ya wateja na watoa huduma katika sekta za Nishati(umeme, petroli na gesi asilia); na Maji (majisafi na usafi wa mazingira).
Miongoni mwa wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Rose Teemba pamoja na Mhe. Robert Makaramba.
Hii ni mara ya tatu kwa IJA kuandaa na kuendesha mafunzo kwa EWURA ambapo kwa mara ya kwanza iliendesha kwa Bodi na mara ya pili kwa Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Aidha, IJA imeendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa mnyororo wa sheria ambapo Oktoba mwaka jana iliendesha mafunzo kwa watumishi wa Benki ya CRDB yaliyolenga kuwajengea uwezo katika kushughulikia changamoto za urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wateja.



