Vigogo 6 wa mahakama kortini fedha za mirathi

GEITA; TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Geita imewafikisha mahakamani watumishi sita wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 261.4 za mirathi.
Watumishi hao wa mahakama na watumishi wanne wa idara zingine za serikali pamoja na wafanyabiashara wanne walifikishwa katika mahakama hiyo na kufunguliwa mashauri matano leo Aprili 30, 2026.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge ametoa taarifa hiyo na kueleza watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia uchunguzi uliofanyika katika akaunti ya Mirathi ya Makakama Kuu Masjala ndogo ya Geita.
Ruge amesema watuhumishi hao waliwalipa wanufaika nane wasio na madai yoyote ya mirathi mahakamani kwa lengo la kurudisha fedha hizo kwa watumishi hao na kwa wenza wao kupitia miamala ya kibenki na simu.
Ametaja watumishi hao wa mahakama ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Veronica Mwanasenga, Ofisa Hesabu Mkuu, Bulemo Mswaga, Ofisa Msaidizi wa Hesabu, Mercy Magezi na Mhasibu, Baldo Kafene.
Watumishi wengine wa mahakama waliofikishwa mahakamani ni Ofisa Msaidizi wa Kumbukumbu Emmanuel Matabaro, pamoja na dereva wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, William Mbwambo.
Ametaja watumishi wanne wa Idara zingine waliohusika ni Tabibu wa Halmashauri ya wilaya ya Winging’ombe mkoani Njombe Upendo Rugohe, Mtumishi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Felix Casmiry.
Ruge ameongeza kuwa watumishi wengine wa idara zingine ni Mhaidroloji wa Wizara ya Maji Dodoma Salimu Lyimo, Diwani wa Kata ya Majengo, Mgema Magembe.
Ruge amewataja wafanyabiashara wanne wanaotuhumiwa kuhusika katika ubadhirifu huo ni Amani Abdallah, Eric Chitumbi, Michael Chanzi na David Mrope.


