Watoa maudhui lishe, afya bila kibali kubanwa

DODOMA; Serikali Imesema inatekeleza Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009 Kifungu Na.173 (1), ambacho kinamtaka mtoa maudhui, mada au matangazo yanayohusu afya ya jamii kupata kibali kutoka kwa waziri wa afya au ofisa aliyeidhinishwa na waziri.
Kauli hiyo imeolewa bungeni leo Na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Hai,Saasisha Mafuwe, aliyehoji serikali ina mpango gani wa kudhibiti watoa elimu ya afya na aina ya ulaji mtandaoni bila kuwa na taaluma inayotambulika jambo linalowachanganya wananchi.
“Serikali inatambua ongezeko la watu binafsi /wataalamu wanaotoa elimu au ushauri wa afya na lishe kupitia mitandao ya kijamii, hali inayoweza kupotosha na kuhatarisha afya za wananchi.
“Hii inatokana na kukua kwa uelewa wa masuala ya lishe, afya, utandawazi na ongezeko la vyombo vya kutolea habari,” amesema Naibu Waziri na kueleza kuwa kushindwa au kwenda kinyume na sheria hiyo mtoa maudhui/mada atachukuliwa hatua za kisheria.



