Mfumo uanagenzi kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya ajira

DAR ES SALAAM: Wadau wa maendeleo ya ujuzi wamepitia na kuthibitisha rasimu ya mwelekeo wa Uanagenzi Tanzania katika hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa mafunzo ya vitendo ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira nchini.
Rasimu hiyo imejadiliwa kwa siku tatu katika kikao kilichoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kupitia Programu ya Global Skills kwa ufadhili wa Serikali ya Norway. Kikao hicho kiliwakutanisha wadau kutoka taasisi za elimu, vyuo vya ufundi, sekta binafsi pamoja na taasisi za serikali.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Programu ya Kukuza Ujuzi kutoka ILO, Hafidh Khamis, alisema rasimu hiyo inalenga kuimarisha mfumo wa mafunzo ya uanagenzi ili kuendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Maeneo ya msingi yaliyojadiliwa ni uratibu wa mafunzo ya uanagenzi, ushirikiano wa wadau pamoja na kuoanisha sera na sheria za Tanzania na mapendekezo namba 208 ya kimataifa kuhusu uanagenzi,” amesema Hafidh.

Kwa upande wake, Mkufunzi na Meneja wa Taaluma wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Mery Maduhu, alisema mfumo wa uanagenzi unahitaji mwanafunzi kupata mafunzo darasani na kwa vitendo sehemu za kazi ili kuongeza uwezo wa kuajirika.
“Mwanafunzi anatakiwa kujifunza chuoni na pia sehemu ya kazi.
Asilimia 40 ya mafunzo hupatikana darasani na asilimia 60 kwa mwajiri kupitia mafunzo kwa vitendo,” amesema Maduhu.
Naye Afisa Rasilimali Watu wa Kituo cha Ubora wa Utalii na Hoteli ya Sansi Zanzibar, Martina Wangoma, aliwataka waajiri kuongeza ushirikiano na taasisi za mafunzo ili kuwasaidia wanafunzi kupata uzoefu wa kazi kabla ya kuhitimu.
“Waajiri wanapaswa kuwapa wanafunzi nafasi zaidi za mafunzo kwa vitendo ili waweze kupata ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira,” amesema Wangoma.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuongeza ajira kwa vijana kupitia mafunzo yanayozingatia mahitaji ya soko la kazi nchini.



