Huduma za dharura Manyara zapunguza hatari ya vifo

MANYARA: UBORESHAJI wa miundombinu ya huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani na dharura mbalimbali, kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa hospitali kutoa huduma za haraka na za kibingwa.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi ameeleza hayo leo Juni 2,2026 baada ya kukagua majengo ya huduma za Dharura na Wagonjwa Mahututi (ICU) katika hospitali hiyo, miradi iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 1.6.

Kihongosi amesema uwekezaji huo umeiwezesha hospitali hiyo kuwa na uwezo mkubwa wa kupokea wagonjwa wa dharura na kuwahudumia kwa wakati, hali ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vilivyokuwa vikisababishwa na kuchelewa kwa huduma za kibingwa.
“Zamani wagonjwa walikuwa wanatoka hapa kwenda KCMC na Muhimbili kutafuta huduma, lakini sasa huduma nyingi muhimu zinapatikana hapa Manyara. Hii ndiyo maana halisi ya kazi na utu; kazi inafanyika na utu wa mwananchi unathaminiwa kwa kusogeza huduma karibu yake,” amesema Kihongosi.

Amesisitiza kuwa uwepo wa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo CT Scan, ICU na huduma za dharura umeongeza uwezo wa hospitali kuokoa maisha ya wagonjwa waliokuwa katika hali mahututi, hususan wa ajali za barabarani.
Ameongeza kuwa kufurahishwa na uwepo wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba (oxygen plant) unaosaidia kuongeza kasi ya matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu.
“Miundombinu hii tuilinde na kuitunza gharama zilizotumika ni kubwa sana, na ikiharibiwa wanaoumia ni wananchi wenyewe, kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha inabaki salama kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” amesisitiza.
Katika taarifa yake ya mradi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Manyara, Yezige Mutajwaa amesema uboreshaji huo umeleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za dharura, hasa katika kupunguza vifo vinavyotokana na ajali na kuchelewa kwa matibabu.

“Majengo haya yamejengwa kwa fedha za Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Rais Samia Suluhu Hassan yameongeza uwezo mkubwa wa kutoa huduma za dharura, ICU na kuokoa maisha ya wagonjwa wengi zaidi kuliko hapo awali,” amesema Dk Mutajwaa.
Ameongeza kuwa uwepo wa huduma hizo umesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za mbali, jambo ambalo hapo awali lilikuwa chanzo cha kuchelewa kwa matibabu na ongezeko la vifo vinavyoweza kuzuilika.
Uboreshaji huo sasa umeifanya kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya huduma za dharura Kanda ya Kaskazini, huku wananchi wakitarajiwa kunufaika zaidi na kupungua kwa vifo vilivyokuwa vikisababishwa na ucheleweshaji wa matibabu.



