Kiswaga ataja changamoto jimboni mbele ya Dk Mwigulu

IRINGA: MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ameibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo lake, ikiwemo migogoro ya ardhi, upungufu wa vituo vya afya, uhaba wa mabweni ya wanafunzi wa kike na changamoto za maji, akiiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuzipatia ufumbuzi.

Kiswaga alitoa maelezo hayo leo mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ifunda jimboni Kalenga, ikiwa ni hitimisho la ziara ya Waziri Mkuu ya jimbo kwa jimbo mkoani Iringa.

Akizungumza katika mkutano huo, Kiswaga alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka mitano iliyopita, bado wananchi wa Kalenga wanakabiliwa na changamoto zinazohitaji uingiliaji wa Serikali ili kuharakisha maendeleo.

Alimpongeza Waziri Mkuu kwa kuamua kufanya ziara ya moja kwa moja kwa wananchi, akisema hatua hiyo imewapa fursa wakazi wa maeneo ya vijijini kueleza changamoto zao na kusikilizwa na Serikali.

“Hili ni jimbo la wakulima na wananchi wake wanategemea sana kilimo. Kufanya ziara ya jimbo kwa jimbo si jambo rahisi, lakini mmetupa nafasi ya kueleza changamoto zetu moja kwa moja,” alisema Kiswaga.

Mbunge huyo alikumbusha kuwa mwaka 2021 aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Kassim Majaliwa, alifanya ziara katika eneo hilo, ziara iliyowezeshwa kupatika kwa zaidi ya Sh Milioni 200 kwa ajili ya maendeleo ya Shule ya Sekondari Ndembela pamoja na zaidi ya Sh Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kilichokuwa changamoto kubwa kwa wananchi.

Alisema tangu wakati huo Kalenga imeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali, ambapo zaidi ya Sh Bilioni 16 zimeelekezwa katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Fedha hizo zimewezesha ujenzi wa shule nne mpya za sekondari, vituo vitatu vya afya, shule mbili za msingi, mabweni ya wanafunzi, madarasa pamoja, vyumba tisa vya maabara na miundombinu mingine.

Aidha, alisema upatikanaji wa umeme umeongezeka kwa kiwango kikubwa, huku vitongoji 67 pekee vikiwa bado havijafikiwa na huduma hiyo.

“Barabara nyingi zimekarabatiwa na nyingine mpya zimejengwa, jambo ambalo limeongeza mawasiliano na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wetu,” alisema.

Kiswaga aliongeza kuwa wiki moja iliyopita jimbo hilo limepokea Sh Milioni 630 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kihanga pamoja na Sh Milioni 583 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika maandalizi ya utekelezaji wa mitaala mipya ya elimu.

Pia Serikali imetoa zaidi ya Sh Milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika shule za sekondari za Lumuli na Lupembewasenga.

Licha ya mafanikio hayo, Kiswaga alisema bado kuna uhaba mkubwa wa mabweni hususan kwa wanafunzi wa kike, hali inayochangia baadhi yao kutembea umbali mrefu kufuata elimu na kuwa katika mazingira hatarishi.

Aliiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa shule za kata na mabweni ili kuongeza kiwango cha ufaulu na usalama wa wanafunzi.

Akizungumzia changamoto za Kata ya Ifunda, alisema wananchi wamelalamikia gharama za kuunganishiwa umeme zinazofikia Sh 320,000 katika baadhi ya maeneo, jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Mbunge huyo pia aliomba majengo yaliyojengwa na TANROADS katika eneo la zahanati ya Ifunda na ambayo kwa sasa hayatumiki, yaelekezwe kutumika kwa shughuli za huduma za afya ili kuongeza uwezo wa kuhudumia wananchi.

Katika sekta ya miundombinu, alisema wananchi wa Wasa na maeneo jirani wanaendelea kukabiliwa na changamoto ya barabara, ingawa alieleza kuwa tayari mwezi Mei mwaka huu mkataba wa ujenzi wa barabara ya Maginga hadi Wasa umesainiwa na matarajio ni kuona utekelezaji wake ukianza kwa wakati.

Hata hivyo, Kiswaga alisema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa tatizo kubwa katika jimbo hilo kutokana na uwepo wa wawekezaji wanaotaka kupata ardhi bila kushirikisha wananchi kupitia taratibu za kisheria.

“Ardhi yoyote inayotolewa bila kufuata utaratibu wa kisheria na bila wananchi kushirikishwa ni lazima waliohusika wachukuliwe hatua. Hakuna mwekezaji anayepaswa kuingia kijijini kupima au kuchukua ardhi bila mikutano halali ya wananchi,” alisisitiza.

Alisema Serikali inapaswa kusimamia kwa karibu uwekezaji ili kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa na migogoro ya ardhi inapungua.

Mbunge huyo pia alieleza kuwa kata tisa kati ya kata 15 za Jimbo la Kalenga bado hazina vituo vya afya vya kutosha wala wodi za kulaza wagonjwa, hali inayowalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma za matibabu.

Aliongeza kuwa changamoto ya maji safi na salama bado ni kubwa katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo na kuiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika miradi ya maji ili kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba aliahidi kuyafanyia kazi maeneo yote yaliyowasilishwa na viongozi pamoja na wananchi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania ili kuharakisha maendeleo na ustawi wa wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button