SUA yajizatiti utafiti wa mbegu bora

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimelekeza nguvu  kuwekeza katika tafiti, ubunifu na teknolojia za uzalishaji wa mbegu bora ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Profesa Maulid Mwatawala amesema hayo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa  Chuo Kikuu hicho wakati akifungua  mjadala wa masuala ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo ya uzalishaji wa mbegu na ubunifu wa teknolojia za kilimo ulioandaliwa na SUA.

Profesa Mwatawala amesema kuwa maendeleo ya sekta ya kilimo yanategemea kwa kiwango kikubwa uwekezaji katika teknolojia rahisi, tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.

“SUA ina watafiti wa mbegu na wameweza kutambulisha mbegu zao na mbegu za aina mbalimbali  ni lazima ziingie sokoni “ amesema Profesa Mwatawala.

Profesa Mwatawala amesema kwa sasa kuna mbegu za mpunga ambazo zitatoa hivi karibu ambazo zinahimili  mabadiliko la tabianchi pamoja na mbegu za maharagwe  ambazo zimesajiriwa hivi karibuni.

“Kwa maana hivi sasa uzalishaji wake utakuwa ni  mkubwa na ikiwa mkubwa  kipato kinakuwa ni kikubwa na jamii inatufaika,”amesema Profesa Mwatawala.

Amesema Chuo Kikuu hicho kimeandaa mjadala wa masuala ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo ya uzalishaji wa mbegu na ubunifu wa teknolojia za kilimo kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wakiwemo watafiti, taasisi za kifedha, wazalishaji wa mbegu na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).

Profesa Mwatawala amesema matumizi ya teknolojia na mbegu bora yanaweza kuongeza uzalishaji wa mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Kwa sasa kuna haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, Serikali na sekta binafsi,”amesema Profesa Mwatawala.

 

Profesa Mwatawala amesema kuwa chuo Kikuu hicho kitaendelea  kutoa mchango wake katika kuzalisha maarifa, teknolojia na wataalamu watakaosaidia kuendeleza sekta ya kilimo na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wakulima kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu,amesema taasisi hiyo imejipanga kuimarisha ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zilizothibitishwa na zenye ubora unaotakiwa.

Chimagu amesema uuzaji wa mbegu feki unahatarisha mafanikio ya wakulima na unaweza kusababisha hasara kubwa katika uzalishaji wa mazao, jambo linaloweza kuathiri juhudi za taifa katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha.

“Hatutasita kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayebainika kukiuka sheria za uzalishaji na uuzaji wa mbegu,”ameonya Chimagu.

Mkurugenzi huyo amesema lengo ni kuhakikishwa wanataka  kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha wanapata mbegu bora zinazowezesha kuongeza uzalishaji wenye tija.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..    https://www.work27.info

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button