Wanafunzi Kibamba Sekondari wapewa elimu ya afya

DAR ES SALAAM: Wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibamba wamejengewa uelewa sahihi kuhusu ugonjwa wa Siko Seli na baadhi yao kuchukua hatua ya kuchunguza hali zao.
Vipimo ‘Screening kits’150 vya uchunguzi wa awali viliandaliwa na jumuiya ya watu wanaoishi na siko seli kwa ajili ya wale wanaohitaji kupima kwa hiyari. viliandaliwa na jumla ya wanafunzi 36 wa Shule ya Sekondari Kibamba wamejitokeza kwa hiari kufanyiwa uchunguzi wa kinasaba cha Siko Seli, mapema hii leo.
Baada ya uchunguzi sita walibainika kuwa wabebaji wa kinasaba (AS), hakuna aliyekutwa na ugonjwa wa Siko Seli (SS), huku wanafunzi wengine 30 wakikutwa na vinasaba vya kawaida (AA).
Tukio hilo limefanyika leo Juni 19, 2026 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Siko Seli Duniani.

Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Ugonjwa wa Siko Seli Tanzania (SCDPCT), imesherehekea siku hiyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kwa pamoja waliwaeleza wanafunzi hao kwa kina kuhusu ugonjwa wa Siko Seli na umuhimu wa kupima mapema ili kufahamu hali za vinasaba.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na waandishi wa habari wamesema elimu hiyo imewasaidia kubadili mtazamo kuhusu ugonjwa huo na kuwaondolea mtizamo hasi dhidi ya wagonjwa wa Siko Seli.
Aidha, wameahidi kuwa mabalozi wa kueneza elimu sahihi waliyoipata katika familia zao na jamii kwa ujumla.
Mwanafunzi, Editha Edward, amesema elimu hiyo imemfundisha kuwa watu wanaoishi na Siko Seli hawapaswi kutengwa bali wanastahili kupendwa, kuheshimiwa na kupewa nafasi sawa katika jamii.

“Nimejifunza wagonjwa wa Siko Seli tusiwatenge, tuwapende na tuwaheshimu ili wasijione kuwa wao si binadamu, bali ni binadamu waliokamilika,” amesema.
Amesema jamii inapaswa kuwaunga mkono watu wanaoishi na Siko Seli ili wasijione wanyonge, waendelee kuchangamana na wengine na kutimiza ndoto zao.
Naye Asnath Mohamed amesema kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa akisikia imani potofu kwamba ugonjwa huu unasababishwa na uchawi, lakini sasa ameelewa kuwa ugonjwa huo hurithiwa kupitia vinasaba vya wazazi.
“Mtaani wanasema mtu mwenye Siko Seli amerogwa, lakini sisi tumepata elimu kutoka kwa madaktari. Tumejifunza kuwa ugonjwa huu hurithiwa kupitia vinasaba vya wazazi. Hivyo mtu hapaswi kupelekwa kwa waganga bali hospitalini. Tusiwatenge watu wenye Siko Seli, tuwapende kama watu wengine,” amesema.
Kwa upande wake, Zacharia Adam amewashukuru madaktari pamoja na mashujaa wa Siko Seli kwa kufika shuleni hapo na kuwapatia elimu pamoja na huduma ya uchunguzi wa kinasaba
Akitoa ushuhuda wake, shujaa wa Siko Seli kutoka SCDPCT, Julius Joseph, amesema bado kuna wanaosema mtu mwenye Siko Seli hawezi kuishi zaidi ya miaka 18.
Amesema kauli za namna hiyo huwakatisha tamaa baadhi ya watu wanaoishi na ugonjwa huo na kuwafanya waache kufuatilia ndoto zao.
“Mimi nina zaidi ya miaka 18, nimesoma na sasa ni Afisa Utabibu. Ndoto yangu ni kuwa daktari,” amesema.
Julius ametoa rai kwa wanafunzi kujitokeza kupima kwa hiari ili kufahamu hali zao za vinasaba mapema, akisema hatua hiyo itawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya maisha.
Naye Afisa Habari wa SCDPCT, Veronica Mrema, amewahimiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wa elimu ya Siko Seli kwa kuifikisha kwa familia na jamii.
“Tumekuja hapa mmesikia ukweli halisi kutoka kwa madaktari bingwa kabisa wa Muhimbili. Tumekuja pia na shujaa wetu, mmemuona na amewaeleza uzoefu wake. Mkirudi majumbani muwe mabalozi wazuri wa elimu kuhusu Siko Seli.
“Tuna vipeperushi tutawapatia. Tunahitaji kwa pamoja tuuvunje mduara wa Siko Seli na tuvunje unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na ugonjwa huu,” amesema Veronica.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mtaalamu wa Sayansi za Maabara wa MNH Wilson Hape, amesema ni muhimu wananchi kupima mapema kabla ya kuamua kuanzisha familia.
“Kwa sababu ukiwa na kinasaba na ukaoana na mtu mwenye kinasaba, ndipo mnapokuwa na uwezekano mkubwa wa kupata mtoto mwenye ugonjwa wa Siko Seli,” amesema.
Ameongeza kuwa wagonjwa wa Siko Seli hukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupungukiwa damu mara kwa mara, hali inayowafanya wahitaji kuongezewa damu hospitalini.
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa hao na wengine wanaohitaji huduma hiyo.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Tuchukue Hatua kwa Usawa: Kuongeza Nafasi ya Kuishi kwa Wagonjwa wa Siko Seli.”
Uongozi wa Shule ya Sekondari Kibamba umeishukuru SCDPCT na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwafikishia wanafunzi elimu pamoja na huduma za uchunguzi wa kinasaba cha Siko Seli, ukieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya maisha na kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii.



