Dk Samia atembelea banda la Vodacom

Kampuni ya Vodacom imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama kinara wa mageuzi ya kidijitali nchini baada ya kutembelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo, katika banda la kampuni hiyo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA), yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walipata fursa ya kujionea na kufahamishwa kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Vodacom Tanzania na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Philip Besiimire. Miongoni mwa huduma hizo ni simu janja zinazowezesha wananchi wengi zaidi kushiriki katika uchumi wa kidijitali, huduma za mawasiliano, huduma za kifedha za M-Pesa pamoja na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazorahisisha maisha ya kila siku ya Watanzania.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Besiimire alisema Vodacom itaendelea kuwekeza katika teknolojia bunifu na suluhisho zinazomweka mteja katikati ili kuongeza ujumuishi wa kidijitali na kuwawezesha wananchi, wafanyabiashara na taasisi kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.
“Dhamira yetu ni kuwaunganisha Watanzania na fursa za kesho. Tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, teknolojia bunifu na huduma jumuishi zinazowezesha watu wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali. Ni heshima kubwa kwetu kupata fursa ya kuwaonesha viongozi wetu ubunifu huu katika maonesho ya SABASABA mwaka huu,” alisema Besiimire.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara na Masoko (Consumer Business Unit Director) wa kampuni hiyo, Brigita Shirima akizungumza kando ya uzinduzi katika banda hilo, alisema maonesho ya SABASABA yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa kampuni hiyo kuwasogezea Watanzania bidhaa na huduma zinazorahisisha maisha yao kupitia matumizi ya teknolojia.
“Kwenye SABASABA ya mwaka huu, tunaonesha namna bidhaa na huduma zetu zinavyoendelea kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia teknolojia. Kuanzia simu janja zinazopatikana kwa gharama nafuu, huduma bora za mawasiliano, M-Pesa hadi suluhisho nyingine za kidijitali, tunaendelea kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki katika uchumi wa kidijitali na kufungua fursa mpya za maendeleo,” alisema Shirima.
Mbali na kuonesha ubunifu wake katika maonesho hayo, Vodacom Tanzania pia ilitunukiwa Tuzo ya Nafasi ya Tatu kwa Mshindi wa Jumla wa Maonesho hayo pamoja na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake mkubwa kama mshirika muhimu wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.
Tuzo hizo zinaakisi dhamira endelevu ya Vodacom Tanzania ya kuendelea kuongoza katika mageuzi ya kidijitali, kupanua upatikanaji wa teknolojia na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kupitia bidhaa na huduma bunifu zinazowawezesha mamilioni ya Watanzania kila siku.



