GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imetoa wito kwa watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kushiriki kufanikisha upatikanaji wa dola milioni moja sawa na sh bilioni 2.6 za Mapambano Dhidi ya Ukimwi.
Mpango huo unatekelezwa kupitia kampeni ya ‘GGML Kili Challenge’ ya kupanda mlima Kilimanjaro kuanzia Julai 24 hadi 30, 2026, ikiwa na kaulimbiu isemayo “Ni jukumu letu sote.”
Kaimu meneja mkuu mgodi wa GGML Duan Campbell alitoa taarifa hiyo juzi katika tamasha la afya lililoandaliwa na GGML la ‘Health Day’ na kueleza kampeni hiyo ilizinduliwa Juni 30, 2026.
Duan amesema kuwa kila mwaka, wawakilishi kutoka GGML, wakandarasi na taasisi mbalimbali za sekta binafsi nchini hukutana kushiriki tukio hilo linalolenga kuhamasisha usalama wa afya.
“Ingawa zoezi la kupanda mlima lina umuhimu wa kiishara, lengo kuu ni kuendelea kuhamasisha jamii na kuunga mkono jitihada za taifa katika mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI”.
Amesema GGML Kili Challenge dhidi ya HIV/AIDS ni mpango wa kitaifa unaoratibiwa na GGML kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kila mwaka ili kudhibiti maambukizi na athari za UKIMWI.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omar Sukari, amesema mkoa unakadiriwa kuwa na watu wapatao 95,000 wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, huku asilimia 80 pekee wakiwa wamefahamu hali zao za maambukizi.
Dk Sukari amesema GGML Kili Challenge mwaka 2025 ilifanikiwa kukusanya Sh milioni 100 ambazo zilitumika katika shughuli za mapambano dhidi ya UKIMWI na kuimarisha afua mbalimbali.
“Tunajivunia kila mmoja aliyejitolea muda wake, nguvu zake na dhamira yake kuiwakilisha GGML katika kampeni hii muhimu”, amesema Dk Sukari.
Katibu Tawala wa wilaya ya Geita, Lucy Beda amesisitiza ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya UKIMWI huku akieleza moja ya hatua ya msingi ni kujenga tabia ya kupima afya na kuchukua tahadhari muhimu za kiafya.
Lucy amesema upimaji wa afya mara kwa mara utasaidia wananchi wote kutambua hali zao mapema, kuishi kwa kujiamini sambamba na kukabiliana na magonjwa katika hatua za awali.
“Naomba tushirikiane na tujitahidi kuchangia. Hakuna fedha ndogo katika kuokoa maisha ya Watanzania na kuimarisha mwitikio wa UKIMWI nchini,” amesema Beda.
Amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa elimu na huduma za afya, hivyo vijana wanapaswa kuongeza juhudi za kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI.



