Serikali yaombwa kuimarisha uhusiano taasisi za vijana

DAR ES SALAAM: Serikali imetakiwa kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazoongozwa na vijana ili kuongeza fursa za ajira, kukuza vipaji vya michezo na sanaa, pamoja na kuharakisha matumizi ya teknolojia na ujasiriamali miongoni mwa vijana nchini.
Wito huo umetolewa na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inua Hub, Jonas Chami, wakati wa uzinduzi wa programu ya Inua Impact Hub jijini Dar es Salaam, akisema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili vijana.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inua Hub, Jonas Chami
Chami alisema Inua Hub ilianzishwa ili kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya kidijitali na ujasiriamali, lakini taasisi hiyo iligundua kuwa kuna kundi kubwa la vijana wenye vipaji vya michezo na sanaa ambao pia wanahitaji kuungwa mkono ili kufikia malengo yao.
Kutokana na hali hiyo, alisema wameanzisha Inua Impact Hub, jukwaa linalowakutanisha mashirika yasiyo ya kiserikali, balozi na wadau mbalimbali kupitia michezo ili kujenga ushirikiano na kubadilishana uzoefu.

Alisema tukio hilo limefanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania baada ya kuanza nchini Portugal mwaka jana, huku likihusisha mashirika mbalimbali yanayotekeleza shughuli za maendeleo ya jamii, yakiwemo yanayopambana na matumizi ya dawa za kulevya.

Chami alisema zaidi ya mashirika 25 yalionesha nia ya kushiriki, lakini toleo la kwanza limefanyika kwa kiwango kidogo ili kupima mwitikio kabla ya kulipeleka katika mikoa mingine ya Tanzania kuanzia mwaka ujao.
Aidha, alisema taasisi hiyo inaendesha mafunzo ya Digital Boot Camps yanayowawezesha vijana kujiajiri na kupata fursa za masomo, mafunzo kwa vitendo (internship) na ajira nje ya nchi kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali za kimataifa.

Katika sekta ya michezo, alisema Inua Hub inalenga kuwa kiungo cha kuwasaidia vijana wenye vipaji kujiunga na akademi na vilabu vya nje ya nchi kupitia ushirikiano wake na wadau mbalimbali wa kimataifa.
Alisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana unahitaji nguvu ya pamoja kutoka Serikalini, taasisi binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha vipaji na ubunifu wa vijana vinachangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Naye, Ofisa wa Kitengo cha Ushirikiano na Mahusiano ya Nje wa Inua Hub, Farida Rashidi alisema lengo la mashindano ni kuwakutanisha taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, kujenga ushirikiano pamoja na kuibua vipaji vya vijana katika michezo na maeneo mbalimbali ya ubunifu.
Akizungumza wakati wa mashindano hayo jijini Dar es Salaam, Farida Rashidi, alisema mpango huo umeanzishwa ili kujenga mahusiano bora kati ya taasisi mbalimbali huku ukiwapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo na vipaji vyao.

Ofisa wa Kitengo cha Ushirikiano na Mahusiano ya Nje wa Inua Hub, Farida Rashidi
Alisema kupitia jukwaa hilo, taasisi zinazoshiriki zinapata nafasi ya kufahamiana, kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kuwasaidia vijana pale wanapobaini kuwa wana vipaji vinavyoweza kuendelezwa.
“Leo tuko kwenye Inua Impact Cup yenye malengo ya kukutanisha taasisi zote za kiserikali na zisizo za kiserikali ambapo lengo letu kuu ni kujenga uhusiano mzuri kati ya taasisi zetu, kuwainua vijana, kuona vipaji vyao na kuwasaidia pale panapokuwa na uwezekano,” alisema.

Farida alisema toleo hilo la kwanza limehusisha jumla ya timu tisa ambazo zote zinawakilisha taasisi mbalimbali, zikiwemo Global Platform Tanzania, Tafeso, Taefi, Acadever na Shadaka.
Alisema mafanikio ya mashindano hayo yameonesha umuhimu wa kuendelea na programu hiyo ili iwe jukwaa endelevu la kuwaunganisha wadau na kuwapa vijana nafasi zaidi za kuonyesha vipaji vyao.

“Hatutarajii hii kuwa mwisho hapa, tunatamani kuendelea zaidi na zaidi kwa sababu tunakuwa tunawainua vijana na kuwapa nafasi ya wao kuonyesha vipaji na ujuzi wao,” alisema.

Aidha, Farida alisema baada ya kubaini vijana wenye vipaji kupitia mashindano hayo, Inua Hub haitawaacha bali itawasaidia kuwaunganisha na watu au taasisi husika kulingana na vipaji walivyonavyo.

Alisema kijana mwenye kipaji cha michezo au ujuzi mwingine atasaidiwa kupata fursa ya kukiendeleza ili baadaye aweze kuchangia katika maendeleo ya jamii.
“Baada ya kugundua vijana wenye vipaji, sisi tunakuwa tunawasaidia kwa kuwakutanisha na watu husika kulingana na kipaji chake.

Hatutawaacha, tutakuwa nao mpaka pale watakapoweza kurudisha mchango wao kwenye jamii,” alisema.




Wow! After all I got a web site from where I be able to actually take valuable
data regarding my study and knowledge.