‘Teknolojia bunifu ziwafikie wakulima, wafugaji vijijini’

MOROGORO: Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa wito kwa wadau wa Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi kuhakikisha kuwa maarifa, teknolojia na ubunifu unaooneshwa katika Maonesho ya Nanenane unawafikia wakulima na wafugaji waliopo vijijini kwa kiwango kikubwa. 

Aidha, Ulega amepongeza juhudi zilizofanyika katika kuendeleza maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kushirikisha sekta binafsi katika kuleta ubunifu na uwekezaji kwenye Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira 2050”.

Ulega ameyasema hayo leo, Agosti 6, 2026, mkoani Morogoro alipokuwa akitembelea Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) ya Kanda ya Mashariki, yaliyowakutanisha wadau wa sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na wafanyabiashara kutoka kanda hiyo.

“Niwasihi wataalamu wetu kuhakikisha kuwa juhudi hizi zinazofanyika hapa hazibakii kwenye maonesho pekee. Maarifa, teknolojia na ubunifu unaooneshwa hapa vinapaswa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili wanufaike,” amesisitiza Ulega.

Pia, Ulega amepongeza makampuni na vikundi vilivyoanzishwa na vijana pamoja na wanawake vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10, ambayo kwa sasa imeongezwa hadi asilimia 15.

 

Amesema hatua hiyo inatia moyo kutokana na namna wanavyotumia fursa hiyo kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kuinua maisha yao.

Waziri Ulega amesisitiza kuwa pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula na bidhaa mbalimbali, ni muhimu kwa wataalamu kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zinapata masoko ya uhakika na kuwafikia walaji kwa wakati.

Kuhusu miundombinu, Ulega amesema Serikali inaendelea na ujenzi na uboreshaji wa barabara na madaraja nchini kwa lengo la kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button