Sekta binafsi zahimizwa kuwekeza katika usafiri wa anga

KILIMANJARO: NAIBU Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika usafiri wa anga ili kuimarisha huduma, kuongeza ushindani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kihenzile ametoa wito huo wakati akikagua maendeleo ya maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ikiwemo Jengo la Watu Mashuhuri la Uhuru, ambalo sehemu yake imekamilika na kuanza kutoa huduma.

Ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika viwanja vya ndege nchini, akisema uwekezaji katika miundombinu ya usafiri wa anga ni muhimu katika kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Rehema Myeya, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha KIA na viwanja vingine vya ndege nchini, kwani inawahakikisha abiria kupata huduma zinazokidhi viwango vinavyohitajika.

“Uwekezaji huu wa Serikali umeleta maboresho makubwa katika miundombinu na huduma za uwanja. Tunaendelea kuona matokeo chanya yanayoongeza ufanisi wa KIA na kuboresha huduma kwa wasafiri,” amesema Mhandisi Myeya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button