Kadogosa amtema kaimu meneja Tanroads Songwe

SONGWE: Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amemuondoa katika nafasi yake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Fredrick Mande, kwa kushindwa kusimamia ipasavyo mradi wa ujenzi wa barabara ya Forodha–OSBP–Tunduma wenye urefu wa mita 1,675 mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Mhandisi Mande ametakiwa kurejea makao makuu ya TANROADS, huku Waziri Kadogosa akisema hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa kumpata meneja mwingine atakayesimamia shughuli za TANROADS mkoani Songwe.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Waziri Kadogosa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo usiku wa Oktoba 15, 2026, akitekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ambaye awali alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo licha ya Serikali kutoa sehemu kubwa ya fedha.

Mradi huo unatekelezwa kwa lengo la kuboresha mtiririko wa magari na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia, kupunguza msongamano, kuongeza ufanisi wa huduma za forodha na kurahisisha biashara za kikanda.
Hata hivyo, utekelezaji wake umeonekana kusuasua licha ya kuwa unatakiwa kukamilika ifikapo Oktoba 31, 2026, kwa mujibu wa mkataba.
Kadogosa amempa mkandarasi wa mradi huo muda wa wiki mbili kukamilisha kazi zilizobaki, huku akiahidi kurejea eneo hilo ndani ya siku saba kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa na kujiridhisha kuwa kasi ya ujenzi imeongezeka.
Aidha, Waziri huyo amewaelekeza Mameneja wote wa TANROADS nchini kuhakikisha kila mradi wa ujenzi unasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa pande tatu zenye majukumu tofauti katika usimamizi wa miradi; msimamizi wa mradi, mkandarasi na msimamizi anayewakilisha Serikali.

Kadogosa ameonya dhidi ya wasimamizi wa miradi kuegemea maslahi ya upande mmoja, akisema mwenendo huo unaweza kudhoofisha usimamizi huru na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Awali, Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, katika ziara yake, alisisitiza kuwa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya miundombinu kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, hivyo watendaji na wakandarasi wana wajibu wa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa huduma iliyokusudiwa.
“Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatoa fedha ili wananchi wanufaike, hivyo tunatakiwa kusimamia kazi ili fedha hizo ziongeze thamani na manufaa kwa wananchi,” alisema Ndejembi.

Ndejembi alisema taarifa alizopokea zilionyesha kuwa mkandarasi alikuwa amelipwa Sh bilioni 4.4 kati ya Sh bilioni 6.8 za mkataba, sawa na zaidi ya asilimia 60 ya thamani ya mkataba, huku maendeleo ya ujenzi yakiwa hayaendani na kiwango cha malipo yaliyofanyika.



