Serikali yaongeza mapambano ya VVU

DODOMA: SERIKALI imeongeza kasi ya mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kuimarisha afua za kinga, upimaji na matibabu, ikiwa na lengo la kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema hayo jana, Oktoba 22, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za kudhibiti VVU na UKIMWI katika mikoa yenye viwango vya juu na vya chini vya maambukizi.
Taarifa hiyo pia imeeleza utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA) kuanzia Januari 2021 hadi Septemba 2026.

Taarifa hiyo iliwasilishwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, ambapo Prof. Kabudi amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali, ikiwemo kufufua kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) kilichopo mkoani Arusha, kinachozalisha dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV), ili kuimarisha upatikanaji wa dawa hizo nchini.
“Serikali pia inaendelea kutekeleza afua za upimaji, usambazaji wa kinga, tohara salama na hiari kwa wanaume, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kupambana na unyanyapaa pamoja na kutoa huduma za matibabu na matunzo,” amesema Prof. Kabudi.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, TACAIDS, NACOPHA, Serikali za Mitaa, asasi za kiraia, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na jamii katika kuongeza uelewa kuhusu VVU, kupunguza unyanyapaa na kuhakikisha huduma za kinga na matibabu zinawafikia vijana, wanawake na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Adam Mrisho, amesema Tanzania imepiga hatua katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU, vifo vinavyotokana na UKIMWI na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Amesema matumizi sahihi ya dawa husaidia kufubaza virusi na kupunguza uwezekano wa maambukizi kwa wengine.
Naye, Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa, ameishukuru Serikali kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu na dawa, akieleza kuwa hatua hiyo inawawezesha watu wanaoishi na VVU kuishi kwa kujiamini.



