Vijana 300 kunufaika ufadhili wa masomo

DAR ES SALAA: Vijana 300 kutoka familia zenye kipato cha chini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya ufundi na ujuzi wa vitendo katika sekta ya kilimo kupitia ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Ushirikiano huo utakaotekelezwa kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo wa Ujuzi-Kwanza unalenga kuongeza fursa za ajira na kujiajiri kwa vijana, pamoja na kuimarisha uzalishaji na minyororo ya thamani katika sekta ya kilimo.

Kupitia mpango huo, vijana watapata mafunzo katika maeneo mbalimbali yakiwemo uzalishaji wa mazao, matengenezo ya vifaa, ufundi wa mitambo ya kilimo na stadi nyingine za kiufundi zinazohusiana na sekta hiyo.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa Oktoba 28, 2026, TBL itagharamia mafunzo hayo, huku VETA ikitoa mafunzo yaliyoidhinishwa na utaalamu wa kiufundi unaotambulika kitaifa.

Aidha, washiriki watapata uzoefu wa vitendo kupitia shughuli za kilimo, ikiwemo kushiriki katika jamii za wakulima wa shayiri na mtama wanaoshirikiana na TBL.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema ushirikiano huo utasaidia kuziba pengo la ujuzi katika sekta ya kilimo na kuwapa vijana nafasi ya kupata mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko.

Alisema kadiri kilimo kinavyoendelea kutumia teknolojia za kisasa, kuna ongezeko la mahitaji ya wataalamu wenye uwezo wa kuendesha na kukarabati mitambo, kuboresha mbinu za uzalishaji na kutoa huduma za kiufundi.

“Ushirikiano huu unafungua fursa kwa vijana wenye vipaji ambao huenda wasiwe na uwezo wa kugharamia mafunzo, huku ukihakikisha kwamba ujuzi wanaoupata unakidhi mahitaji halisi ya sekta,” alisema Kasore.

Takwimu zinaonesha kuwa kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 26.3 ya pato la taifa kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2024, huku kikiendelea kuajiri zaidi ya nusu ya watu wote wanaofanya kazi nchini.

Hata hivyo, mabadiliko ya sekta hiyo kuelekea matumizi ya teknolojia za kisasa yanaongeza hitaji la wataalamu wenye ujuzi katika uzalishaji, umwagiliaji, usimamizi wa mazao baada ya kuvunwa na uendeshaji wa mitambo ya kilimo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alisema uwekezaji katika mafunzo ya vitendo kwa vijana ni muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima na jamii zinazozunguka shughuli za uzalishaji.

Alisema sehemu kubwa ya malighafi zinazotumiwa na kampuni hiyo hutokana na mazao yanayolimwa nchini, hivyo maendeleo ya biashara yake yanahusiana na uwezo wa wakulima kuzalisha kwa tija.

“Kwa kuwekeza kwa vijana wanaopata ujuzi wa vitendo katika kilimo, tunatengeneza fursa za ajira na ujasiriamali, huku tukiimarisha thamani inayowezesha Watanzania kujipatia kipato na kuendeleza biashara yetu,” alisema Kilpin.

Kwa mujibu wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, zaidi ya vijana 800,000 huingia katika soko la ajira nchini kila mwaka, hali inayoongeza umuhimu wa kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi na kuwaandaa vijana kujiajiri.

Utafiti wa ufuatiliaji wa wahitimu uliofanywa na VETA umeonesha kuwa asilimia 75 ya wahitimu walikuwa wameajiriwa au kujiajiri, huku kujiajiri kukichukua sehemu kubwa zaidi ikilinganishwa na ajira rasmi.

TBL imekuwa ikishirikiana na wakulima wa Tanzania tangu mwaka 1933, ambapo kwa sasa inanunua shayiri na mtama kutoka kwa wakulima wadogo zaidi ya 2,500 katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma.

Kampuni hiyo pia huwapatia wakulima mbegu, mafunzo ya kilimo na masoko ya uhakika. Aidha, uwekezaji wake katika uchakataji wa shayiri nchini kupitia Kiwanda cha Kilimanjaro Malting kilichopo Moshi uliwezesha kiwanda hicho kukamilisha mwaka wake wa kwanza wa uzalishaji kamili mwaka 2025 kwa kutumia shayiri iliyolimwa nchini.

Akizungumzia upanuzi wa huduma za VETA, Kasore alisema idadi ya wanafunzi waliojiunga na mafunzo imeongezeka kutoka 69,347 mwaka 2022/23 hadi 116,468 mwaka 2025/26, huku vyuo vipya 65 vikitarajiwa kufunguliwa Januari 2027.

Alisema ushirikiano na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na kwamba taasisi hizo zitafuatilia maendeleo ya wahitimu wa mpango huo ili kupima matokeo yake.

Mpango wa Ujuzi-Kwanza unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, Ajenda ya 10/30 inayolenga kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030, pamoja na programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora inayohamasisha vijana kushiriki katika biashara za kilimo.

Kilpin alisema mafanikio ya mpango huo hayatapimwa kwa idadi ya vijana watakaopata mafunzo pekee, bali pia uwezo wao wa kutumia ujuzi huo kujiajiri, kuanzisha biashara na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button