Mbarawa: Hakuna anayetudai SGR

TABORA: WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema hakuna mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) katika kipande cha Makutupora mkoani Singida hadi Tabora anayeidai Serikali, akisisitiza kuwa mradi huo hauna changamoto ya fedha.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo katika eneo la Nyahuha, mkoani Tabora, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa reli hiyo, ambapo alieleza kuwa changamoto iliyokuwepo awali ilikuwa uwezo wa mkandarasi kupanga na kutekeleza kazi kwa kasi inayotakiwa ili kuwasilisha madai ya malipo kwa wakati.

Alisema Serikali imehakikisha fedha za kutosha zinapatikana kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupatikana kwa Sh trilioni 3.67 mwaka jana kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.

“Mradi huu hauna changamoto ya fedha kwa sababu mwaka jana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alituwezesha kupata Sh trilioni 3.67. Kwa kweli hakuna shida ya fedha, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuwezesha kupata fedha hizo,” alisema Profesa Mbarawa.

Alifafanua kuwa kuwepo kwa fedha pekee hakumaanishi malipo yanaweza kufanyika bila mkandarasi kutimiza taratibu zinazotakiwa, ikiwemo kuwasilisha hati za madai ya malipo zinazojulikana kama Interim Payment Certificates (IPC).

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mkandarasi alikuwa akikabiliwa na changamoto ya kuzalisha na kuwasilisha IPC za kutosha kulingana na kiwango cha kazi kilichotekelezwa, hali iliyochangia kuchelewa kwa mchakato wa malipo.
“Hapa hakuna shida ya fedha. Shida kubwa iliyokuwepo ni mkandarasi mwenyewe alikuwa hana uwezo wa kuzalisha IPC za kutosha,” alisisitiza.
Profesa Mbarawa alisema kwa sasa kuna matumaini ya kuimarika kwa utekelezaji wa mradi huo kutokana na utaratibu wa kazi uliowekwa na uwezo ambao mkandarasi ameonyesha katika shughuli zake.

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa alizotoa, hati ya madai ya malipo iliyowasilishwa ina tarehe ya mwisho ya Novemba 6, na Serikali italipa kabla ya muda huo kukamilika.
Alisema matarajio ya Serikali ni kuona kazi zikiendelea kwa kasi inayotakiwa ili kukamilisha mradi kwa wakati uliopangwa.
Aidha, Profesa Mbarawa alieleza kuwa Serikali inalenga kufikia hatua za mwisho za ujenzi wa kipande hicho cha tatu ifikapo mwaka 2028, hatua itakayowezesha kuanza kwa majaribio ya reli hiyo ya kisasa.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia maendeleo ya mradi huo ili kuhakikisha mkandarasi anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mipango iliyowekwa na kwamba ujenzi unaendelea bila vikwazo visivyo vya lazima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Shiwa alisema TRC inaamini kuwa mgawanyo wa mradi katika sehemu tano na usimamizi adhubuti wa ratiba ya utekelezaji vitawezesha kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha reli ya kisasa kutoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button