Mitambo 41 yarudishwa baada ya agizo la Kadogosa

SHINYANGA: Agizo la Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, alilolitoa Oktoba 2026 mkoani Shinyanga, limeanza kutekelezwa baada ya vifaa na mitambo ya ujenzi kuanza kurejeshwa katika maeneo ya miradi husika, hatua inayolenga kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi na kukamilika kwa wakati.

Waziri Kadogosa alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Msalala, wilayani Kahama, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha vifaa na mitambo inayohitajika katika utekelezaji wa miradi inapatikana na kubaki katika maeneo ya kazi ili kuepusha ucheleweshaji.

Alieleza kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya wakandarasi kuhamisha vifaa na mitambo kutoka mradi mmoja kwenda mwingine kwa lengo la kukidhi masharti ya malipo ya awali ya maandalizi ya mradi, yanayojulikana kama ‘Mobilization’.

Kwa mujibu wa Waziri Kadogosa, tabia hiyo inaweza kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati na kuisababishia Serikali gharama zisizo za lazima, ikiwamo kulipia tena usafirishaji wa vifaa na mitambo kutoka eneo moja kwenda jingine.

Utekelezaji wa agizo hilo umeanza pia katika mradi wa ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass), yenye urefu wa kilomita 7.3.

Hadi Oktoba 29, 2026, mkandarasi wa mradi huo alikuwa amerejesha mitambo 41 kati ya 65 inayohitajika kwa mujibu wa mkataba, sawa na asilimia 63 ya mitambo iliyotakiwa kuwepo katika eneo la mradi.

Aidha, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ulimwita mkandarasi huyo katika kikao cha kawaida cha mradi kilichopangwa kufanyika Oktoba 30, 2026, kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa kuendelea na utekelezaji wa kazi mara baada ya kurejesha mitambo hiyo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mitambo inayohitajika inabaki katika eneo la mradi na hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, kuzuia ucheleweshaji na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button