Wageni AFCON kunufaika mfumo malipo ya kidijitali

DAR ES SALAAM: Wananchi na wageni watakaoingia nchini wakati wa mashindano ya AFCON watanufaika na kurahisishwa kwa huduma za mafuta, gesi na mahitaji mengine ya magari kupitia mfumo wa malipo ya kidijitali unaolenga kuongeza usalama na kurahisisha usimamizi wa matumizi.

Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania imezindua mfumo mpya wa kadi za malipo za kidijitali utakaotumika katika vituo vyake 130 vilivyosambaa nchini, ukiwawezesha wateja kulipia huduma mbalimbali kupitia mfumo mmoja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa kampuni hiyo, Getrude Mpangile, amesema mfumo huo umeboreshwa ili kuwawezesha wateja kulipia mafuta, gesi, huduma za kubadilisha mafuta ya injini na kuosha magari.

Amesema kupitia programu ya TotalEnergies Mobility, watumiaji wataweza kufuatilia miamala na matumizi yao kwa wakati, hatua inayolenga kuongeza uwazi na udhibiti wa matumizi.

Mfumo huo pia unaendana na juhudi za kukuza matumizi ya teknolojia katika sekta binafsi na kuboresha utoaji wa huduma, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kuimarisha uchumi, kuvutia uwekezaji na kupanua fursa za biashara.

Kwa upande wao, watumiaji wa kadi hizo, Nishit Mdessa na Thabit Binzou, wamesema mfumo huo unarahisisha usimamizi wa matumizi, kuongeza usalama na kupunguza uwezekano wa matumizi ya mafuta yasiyoidhinishwa.

Wamesema mfumo huo unatarajiwa kuwa na manufaa kwa wasafiri na wadau wa utalii, hususan katika kipindi cha AFCON, ambapo idadi ya wageni na mahitaji ya huduma za usafiri yanatarajiwa kuongezeka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button