Mvua yatikisa Kigoma, nyumba 121 zaathirika

KIGOMA; NYUMBA 121 na makanisa manne zimeezuliwa paa, huku nyingine zikiharibika kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo kwa kipindi cha mwezi mmoja tangu kuanza kwa mvua hizo, zaidi ya kaya 100 zimeathirika.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hashim Mvogogo, alitoa taarifa hiyo wakati akimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ambaye aliongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Kamati ya Maafa kukabidhi misaada iliyotolewa na halmashauri kwa waathirika wa mvua hizo.
Mvogogo alisema kata zilizoathirika zaidi ni Gungu, ambako nyumba 70 zimeathirika, Kibirizi nyumba 47, Mwanga Kusini nyumba mbili na Katubuka nyumba mbili.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, halmashauri imewasilisha tani 2.6 za mchele, tani 1.9 za unga wa mahindi, tani moja ya maharage pamoja na sukari, mafuta ya kupikia na sabuni za kufulia.
Aliongeza kuwa halmashauri inaendelea kushughulikia mahitaji mengine ya waathirika, ikiwamo magodoro, shuka, blanketi na maturubai, huku baadhi yao wakihifadhiwa katika maeneo mbalimbali.
Akikabidhi misaada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, aliwataka wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Serikali kwa kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha nchini.
Balozi Sirro alisema tayari maeneo hatarishi yametambuliwa na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wameelekezwa kuhama kwa ajili ya usalama wao.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikaidi kuhama na kubeza tahadhari zinazotolewa kuhusu mvua hizo, akisisitiza kuwa Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaokaidi maelekezo ya mamlaka.
Pamoja na hayo, alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua na kuwasaidia wananchi watakaoathirika na mvua hizo, akieleza kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa inayotarajiwa kupata mvua nyingi.
Alisema tangu Oktoba, wilaya za Kigoma, Buhigwe, Kakonko, Kasulu na Kibondo zimekumbwa na mvua kubwa zilizoambatana na upepo na kusababisha madhara kwa wananchi.
Baadhi ya waathirika, akiwamo Kobwa Kamana, waliishukuru Serikali kwa msaada wa vyakula walioupata, lakini wakaomba iongeze msaada wa vifaa vya ujenzi, hususan bati, ili kuwawezesha kurejea katika makazi yao.



