Watendaji uchaguzi wasisitizwa uadilifu

DODOMA: Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, amewataka watendaji wa uchaguzi kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni za uchaguzi ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Mwambegele ametoa wito huo leo, Novemba 2, 2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yanayolenga kuwaandaa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chamwino na uchaguzi wa kata 11 za Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwambegele amesema watendaji wanapaswa kuzingatia viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kufuata Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni za maadili na maelekezo yanayotolewa na tume.

“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema.

Amewaasa watendaji hao kutofanya kazi kwa mazoea licha ya baadhi yao kuwa na uzoefu wa kusimamia chaguzi zilizopita, akieleza kuwa kila uchaguzi una mazingira na taratibu zake zinazopaswa kuzingatiwa.

Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026, katika Jimbo la Chamwino na kata 11 za Tanzania Bara.

Kata hizo ni Nonde katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge (Halmashauri ya Mji Njombe), Bargish (Halmashauri ya Mji Mbulu), Makole (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza), Mwera (Halmashauri ya Wilaya ya Pangani) na Oldonyosambu (Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro).

Nyingine ni Igalula katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shelui (Halmashauri ya Wilaya ya Iramba), Mvumi (Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa), Nyarero (Halmashauri ya Wilaya ya Tarime) na Ilolangulu (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button