RAY C, Lulu wamfagilia Zuchu kuhudumia wageni

DAR ES SALAAM: Msanii wa filamu Elizabeth Michael maarufu kama Lulu na yule wa muziki Rehema Chalamila ‘Ray C’, wamempongeza mwimbaji Zuhura Othuman ‘Zuchu’ kwa kuonesha ukarimu na kuthamini mila na desturi za Kitanzania baada ya kuwahudumia nyumbani kwake msanii wa Nigeria, Davido na mkewe Chioma.
Zuchu amezungumziwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akitimiza majukumu ya kuwahudumia wageni hao nyumbani kwake, jambo ambalo limeibua mjadala kuhusu nafasi ya mwanamke katika familia na namna ya kuwapokea wageni.
Akitoa maoni yake, Lulu memtetea Zuchu dhidi ya wanaomkosoa kwa kitendo hicho, akisisitiza kuwa kuwahudumia wageni nyumbani si jambo la kulaumiwa, bali ni sehemu ya ukarimu na ustaarabu.
Kwa upande wake, Ray C pia amempongeza Zuchu, akivutiwa na namna alivyoweza kutofautisha maisha yake ya umaarufu jukwaani na majukumu yake anapokuwa nyumbani.
“Mwanamke aliyefundwa utamjua tu kwa matendo yake! Kauvua umaarufu wa stejini, kauvaa uhusika wa nyumbani kama mke mbele ya wageni,” amesema Ray C.
Ameongeza kuwa kitendo hicho kinaakisi maadili ya Kitanzania ya kumkaribisha na kumjali mgeni anapofika nyumbani.



