Tanzania kukabidhi CAF ofisi za AFCON 2027 kesho

DAR ES SALAAM: Tanzania kesho, Novemba 25, 2026, itakabidhi rasmi ofisi za Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kwa ajili ya kutumika kama Makao Makuu ya Maandalizi ya Mashindano ya AFCON 2027.
Sherehe za makabidhiano hayo zitafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 3:00 asubuhi, ambako ofisi hizo zimejengwa.
Tukio hilo pia litahusisha utiaji saini wa mkataba wa udhamini wa matangazo kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na CAF, utakaoiwezesha TTB kuwa mshirika rasmi wa mashindano hayo.
Makabidhiano hayo ni sehemu ya maandalizi ya pamoja ya Tanzania, Kenya na Uganda ya kuandaa AFCON 2027, mashindano yanayotarajiwa kuunganisha wadau na mashabiki wa soka barani Afrika huku yakitangaza Afrika Mashariki duniani.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imewaalika wananchi kufuatilia tukio hilo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.



