Zanzibar yapata gawio la bil 52/-

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema hadi mwezi uliopita Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepata gawio la Sh bilioni 51.7.

Dk Jafo amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24.

Aliwaeleza wabunge kuwa fedha hizo za misaada ya kibajeti kutoka nje zilizopelekwa SMZ. Kuhusu fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo Zanzibar, alisema wizara hiyo imeendelea kufanya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za mfuko huo kwa majimbo 50 ya Zanzibar.

Dk Jafo alisema hadi kufikia Machi mwaka huu Sh bilioni 1.4 zilipelekwa Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Jimbo.

“Serikali imeendelea kuwawezesha wananchi wa pande zote mbili za Muungano kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo, miradi na programu hizo zimefanikiwa kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii,” alisema.

Aidha, kuhusu kuratibu masuala yasiyo ya Muungano ili kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na SMZ, ofisi hiyo imeendelea kuhimiza umuhimu wa Wizara au idara na taasisi zisizo za Muungano kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu, sera, sheria, utaalamu na wataalamu.

Dk Jafo alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, vikao 12 vya ushirikiano vimefanyika kati ya Wizara au Taasisi na Idara za SJMT na SMZ, pia elimu kwa umma kuhusu umuhimu na faida za Muungano imetolewa kupitia redio, runinga, magazeti, machapisho au vipeperushi, Jarida la Ofisi ya Makamu wa Rais na Mitandao ya Kijamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button