NCAA waja na mbinu mpya kuvutia watalii

KATIKA kuhakikisha wanavuka malengo ya watalii wa ndani Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imekuja na mbinu mpya ya kuwavutia watalii wa ndani katika kipindi cha Sikukuu ya X-Mass na mwaka mpya kwa kutoa vifurushi vipya vya bei rafiki kwa watalii wa ndani kwenda kutalii katika hifadhi ya Ngorongoro.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Utalii na Huduma za Masoko (NCAA) Mariyamu Kobelo katika mkutano wake na waandishi wa habari Arusha.
Amesema katika kipindi cha julai hadi Novemba mwaka huu watalii wa ndani 2000 wameshatembelea Hifadhi ya Ngorongoro tofauti na miaka ya nyuma.
Meneja huyo amesema kutokana hali hiyo wanaamini kabisa katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia jana Desemba 4 mwaka huu hadi Januari 4 mwakani wanaweza kuvuka malengo ya watalii wa ndani kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Amesema katika kuchagiza hilo linafanikiwa uongozi wa NCAA umekuja na kitu kipya cha kuhamashisha utalii wa ndani kinachojulikana kwa jina la ‘’Merry & Wild Ngorongoro Awaits’’ ambacho kitakuwa na vifurushi vitatu vya bei rafiki kwa watalii wa ndani vitakavyojulikana kwa jina la faru Sh 450,000,Tembo shilingi 130,000 na chui Sh 85,000 vimejumuisha gharama za usafiri na malipo ya ndani ya hifadhi.
Meneja huyo amesema eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lina vivutio vingi ambavyo wananchi wa Tanzania bado hawajavijua hivyo ni wakati wa kutalii hifadhi hiyo ili kujionea wenyewe vivutio hivyo ni pamoja na Bonde la Ngorongoro, Embakai, Ndutu, Olduvai na mapango ya kale.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha ,Missaile Mussa amesema Serikali ya Mkoa wa Arusha unaungana na uongozi wa NCAA katika kuzindua kampeni hiyo ya kuwavutia watalii wa ndani lengo likiwa kuwavutia watalii hao kujionea vivutio vilivyoko katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Mussa aliwakilishwa na Katibu Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Arusha, Daniel Loiruck amesema hiyo ni fursa kwa watanzania kwenda kwa wingi katika Hifadhi ya Ngorongoro ili mamlaka hiyo iweze kujiendesha na serikali kuongeza mapato kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.




