Tanga wana deni kwa Rais Samia

RAIS Samia Suluhu Hassan anaendelea na ziara yake ya siku saba mkoani Tanga ambayo ilianza tangu Februari 23, mwaka huu na inatarajiwa kukamilika Machi Mosi.
Kwa mujibu wake wakati anaanza ziara hiyo katika mji wa Mkata wilayani Handeni mchana wa Jumapili ya Februari 23, Rais Samia alieleza kuwa ziara yake mkoani humo ni kukagua utekelezaji wa miradi ya Sh trilioni 3.1 ambazo zimetolewa na serikali yake kwa ajili ya maendeleo, pamoja na kuwasalimia wananchi wake.
Tangu aanze ziara hiyo, kumekuwapo na uthibitisho wa dhahiri wa jinsi fedha hizo za maendeleo zilivyofanya kazi
kubwa ya kuwaletea maendeleo wakazi wa Tanga, ambako wao binafsi na wawakilishi wao (wabunge), wametoa ushuhuda kuonesha jinsi Rais Samia kupitia serikali anayoiongoza, alivyofanya makubwa Tanga.
Katika sekta zote, kazi kubwa imefanywa na serikali kuanzia elimu hadi sekta za uzalishaji mali na uchumi kama vile uvuvi na uchumi wa buluu.
Kwa mfano, serikali imejenga majengo mazuri ya utawala katika halmashauri za Bumbuli na Mji wa Handeni, Hospitali ya Wilaya ya Handeni ambayo sasa itakuwa maalumu kwa tiba ya mifupa, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Sayansi, miradi ya maji, miradi ya barabara ikiwamo ya Bagamoyo –Pangani, ugawaji wa boti za uvuvi na ugawaji wa mitungi ya gesi kwa ajili ya nishati safi ya kupikia.
Lakini ukiacha hiyo mikubwa ambayo Rais Samia ameizindua na mingine kuiweka mawe ya msingi, kuna mingine iliyokamilika kama ujenzi wa shule za sekondari za kata, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, ujenzi wa barabara, ukamilishaji wa miradi ya maji, na kupeleka rasilimaliwatu katika sekta mbalimbali.
Kwa hiyo, unaposikiliza wabunge na wananchi kwa ujumla katika ziara hii ya Rais Samia mkoani Tanga, unapata
uthibitisho wa jinsi alivyoleta mapinduzi makubwa katika mkoa huo ndani ya miaka minne ya uongozi wake.
Ni dhahiri kuwa wananchi wa Mkoa wa Tanga wana deni kubwa kwa Rais Samia na serikali yake, na jinsi ya kulilipa
ni pamoja na kulinda miundombinu yote iliyowekezwa na serikali na pia kutunza mali nyingine zilizotolewa kama vile boti kwa wavuvi wa mkoa huo, na majengo ya utawala kwa watumishi wa umma na wananchi.
Kubwa jingine ni kwa wananchi kuhakikisha wanalinda amani na utulivu nchini ili serikali iendelee kuwaletea
maendeleo kwa sababu amani na utulivu vinapokosekana, maana yake hakuna jambo la maendeleo linaloweza kufanyika.
Kwa makubwa haya ya serikali ya Rais Samia ni dhahiri anastahili kuendelea kuungwa mkono katika kuwatumikia
wananchi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla na hilo litafanyika kwa kutumia fursa anazowekeza kwa wananchi wake, ili kujiletea maendeleo wao wenyewe na kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.