Kila la heri EAC maonesho ya utalii Berlin

MAONESHO ya Kimataifa ya Utalii (ITB) yanaanza leo katika Jiji la Berlin, Ujerumani na yatafanyika kwa siku tatu hadi Machi 6.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inashiriki maonesho hayo makubwa ya biashara ya utalii duniani ikiwa ni mara ya kwanza.
Yanatarajiwa kuileta sekta ya utalii pamoja na kupatia ufumbuzi changamoto zinazorudisha nyuma sekta hiyo ndani ya jumuiya na duniani kwa ujumla.
Katika maonesho hayo, EAC itaonesha vivutio vyake chini ya kaulimbiu ya ‘Tembelea Afrika Mashariki upate furaha’ huku ikieleza kinaubaga vivutio vinavyopatikana ndani ya mipaka ya EAC.
Mbali ya Sekretarieti ya EAC, mataifa wanachama yanayotarajiwa kushiriki katika maonesho hayo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu kwa nchi wanachama kujiimarisha katika utalii, tunahimiza zishiriki kikamilifu sambamba na wadau wakitanguliza maslahi ya nchi zao pamoja na EAC ili kujihakikishia kunakuwapo soko la uhakika katika mataifa tofauti.
Tunaliona hili kama fursa adhimu kibiashara ambayo nchi wanachama zinapaswa kuichangamkia kutokana na ukubwa wa maonesho hayo ambayo yatakusanya wadau wa utalii kutoka duniani kote.
Tunaamini maonesho yatatoa nafasi ya kubadilishana mawazo na teknolojia pamoja na kujifunza mbinu bora za kusimamia sekta husika.
Mbali na biashara ya utalii, maonesho hayo yatakuwa na dhima maalumu ya kutangaza utamaduni, historia, utajiri na mandhari ya kupendeza ya nchi wanachama hatua itakayosaidia nchi za EAC kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji.
Ni wazi kwamba ushiriki wa EAC utavutia watalii na wawekezaji wa kimataifa watakaoangazia urithi wa kitamaduni
wa watu wa Afrika Mashariki, uzuri wa asili na vivutio vya kipekee.
Maonesho hayo pia yatatoa fursa muhimu ya kukutana na wadau wa utalii kama vile wasafirishaji, wamiliki wa hoteli na waendeshaji wa shughuli za utalii ambapo mbali na kubadilishana uzoefu, watatengeneza mtandao mzuri utakaotumika kuwaleta watalii ndani ya EAC.
Ni bayana kwamba ushiriki wa nchi zote wanachama wa jumuiya utasaidia kutangaza vivutio vilivyomo katika kila nchi hali itakayopanua soko la utalii kwa nchi mojamoja na kwa jumuiya kwa ujumla.
Tunategemea vivutio vya utalii kama vile mbuga za wanyama zikiongozwa na Mbuga ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro na vinginevyo katika nchi nane wanachama wa EAC, vitaendelea kutangazwa na kupigiwa debe vizidi kujulikana duniani na kuvutia watalii wengi.
Hivyo basi, ni jukumu la kila nchi za EAC kuchangamkia maonesho haya na kuhakikisha yanatumika kama jukwaa la kuleta mapinduzi katika sekta ya utalii ambayo ni mhimili wa uchumi.
Tunaitakia kila la heri EAC katika ushiriki wake wa kwanza kwenye maonesho hayo ambayo pia ni fursa muhimu ya kujenga mustakabali bora wa sekta ya utalii na kuleta maendeleo kwa nchi wanachama hali itakayoinua uchumi wa wananchi wa eneo husika na kupandisha pato la nchi na EAC kwa ujumla.



