Tunaitakia ufanisi Bodi ya Ithibati ya Wanahabari

BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ilizinduliwa juzi Dar es Salaam kwa kupewa maagizo saba ya kutekeleza.

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alizindua bodi hiyo yenye wajumbe wanne akiisisitiza ihakikishe wanahabari wote wanazingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia taaluma.

Kuzinduliwa kwa bodi hiyo iliyoundwa mwaka jana na serikali, ni hatua muhimu katika kuimarisha tasnia ya habari nchini.

Tunaamini kwamba chini ya uongozi wa mwanahabari mkongwe, Tido Mhando, bodi itatekeleza jukumu lake kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma.

Pia, upande wa wajumbe wa bodi, hakuna shaka kwamba wameteuliwa kwa kuzingatia umahiri wao katika tasnia ya habari. Wana uzoefu ambao tuna imani watakuwa chachu katika kuimarisha viwango vya uandishi wa habari nchini.

Kuwapo kwa chombo hiki cha kutoa mwongozo na tathmini kwa wanaofanya kazi katika sekta hii muhimu, tunaiona  ni fursa kwa waandishi wa habari kujiendeleza na kuzingatia maadili.

Tunapongeza hatua ya serikali kuona umuhimu wa kuwapo chombo hiki na kukizindua rasmi kwa kuwa kina nafasi ya kipekee ya kukuza tasnia ya habari yenye uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini.

Ni matumaini yetu bodi itachangia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha heshima ya tasnia kwa kuhakikisha kuwa waandishi wanafuata kanuni za uandishi wa habari na kuzingatia maadili ya kitaaluma.

Aidha, bodi hii iwe chachu katika kukabiliana na changamoto ambazo tasnia ya habari inakumbana nazo, hususani uvunjwaji wa haki za waandishi na zihusuzo uhuru wa kupata habari.

Kuanzishwa kwa bodi hii ni dalili ya matumaini, kwani inatoa fursa kwa waandishi kujihusisha na mchakato wa kuimarisha haki zao na kuanzisha mazungumzo kati yao na serikali.

Tuna matumaini kwamba bodi hii itashirikiana na wadau wengine, kama vile vyombo vya habari na mashirika ya kiraia, ili kufanikisha malengo yake.

Tunawataka wajumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari wafanye kazi kwa uaminifu na kwa kujituma, huku wakizingatia maadili na viwango bora vya uandishi.

Tuna imani kwamba kwa juhudi zao, tasnia ya habari nchini itakua na kuwa na heshima kubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Huu ni wakati wa kuimarisha uhuru wa habari na kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu. Tunawatakia ufanisi mwema katika majukumu yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button