Viongozi washauri ushirikiano upatikanaji nishati endelevu
Viongozi mbalimbali wanaoshiriki mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi ya nishati endelevu kwa watu wote unaofanyika Barbados wameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa nishati endelevu kwa gharama nafuu.
Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika mji mkuu wa nchi hiyo, Bridgetown, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Tanzania kwa upande wake chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, imepanga kuwawezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema kupitia mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115 utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu kwa maendeleo na ustawi wa wananchi katika ngazi mbalimbali.
Dk Biteko amesisitiza kuwa, utekelezaji wa lengo namba 7 katika mpango wa maendeleo ya milenia unahitaji ushirikiano miongoni mwa Serikali na sekta binafsi katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi ikiwa ni moja ya utatuzi wa changamoto zilizopo.

Amesema ni muhimu kwa mataifa kuwekeza katika miundombinu kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi sambamba na kuweka mifumo ya ubunifu na utashi katika kuwezesha upatikanaji wa nishati kwa usawa bila kuacha makundi mengine.
Naye, Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley amesema ni wakati sasa wa kuweka mkakati wa kimataifa na kukubaliana kushirikiana kumaliza changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa wote.

Akizungumzia mkutano wa misheni 300 (M300) uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mia amesema inatia simanzi kuwa na watu zaidi ya milioni 600 barani Afrika wanaishi bila huduma ya umeme suala ambalo limesababisha changamoto katika nchi nyingi duniani.
“Tunahitaji kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo, uwe ufumbuzi wa ndani au kutoka katika nchi yoyote duniani,” amesema Mottley.



