Serikali kuboresha miundombinu uzalishaji mbegu za kilimo

DODOMA: SERIKALI imekusudia kuboresha miundombinu ya uzalishaji mbegu bora za kilimo hususan mahindi, alizeti, maharagwe na mimea ya kunde.
Vilevile itaboresha miundombinu ya uzalishaji viumbe maji ili kupata vifaranga na chakula cha samaki chenye ubora stahiki, upunguzaji upotevu wa mazao ya samaki na uvuvi wa bahari kuu pamoja na kuwezesha kaya duni 260,000 kwa miaka sita mfululizo.
Kaya hizo ambazo ni sawa na watanzania 1,300,000 katika mikoa 11 ya Tanzania Bara zinajengewa uwezo kupitia programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) katika mradi unaolenga kuimarisha mifumo jumuishi ya usalama wa chakula na lishe kwenye halmashauri 41 zinazounda mikoa hiyo.
SOMA ZAIDI: Kilimo kuwa chanzo kikubwa pato la taifa
Ili kuwezesha utekelezaji chanya wa program ya AFDP, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu ambayo inaratibu program hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambao ni watekelezaji imewakutanisha makatibu tawala wa mikoa yote 11, pamoja na maofisa viungo kwenye halmashauri husika ili kuwajengea uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa program hiyo.

Akifungua kikao kazi hicho kinachoendelea mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa (TAMISEMI) Beatrice Kimoleta, amewasisitiza watendaji hao kusimamia kikamilifu pesa zote zitakazotolewa kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa mradi akikemea ubadilishwaji wa matumizi ya pesa za miradi.
SOMA ZAIDI: Mashirika ya umma Afrika yawekeze kilimo
“Hapa naomba nisisitize hizi pesa zisitumike kinyume na taratibu zilizoelekezwa katika utekelezaji wa program hii, Serikali inahitaji kuona matokeo chanya kama inavyolengwa na programu, isitokee mkabadilisha hata shilingi ya matumizi ya pesa hizi, kufanya hivyo itakuwa ni kama dhuruma kwa walengwa, na sitarajii mtu yeyote kubadilisha matumizi,” amesisitiza Kimoleta.

Awali akitoa taarifa ya programu hiyo, Salimu Mwinjaka ambaye ni mratibu wa program hiyo ya AFDP ameitaja mikoa itakayonufaika na program hiyo kuwa ni Morogoro, Manyara, Singida, Dodoma, Tabora, Mwanza, Lindi, Pwani, Shinyanga, Geita na Tanga.
Aidha amesema tamati ya programu ya AFDP serikali inatamani kuona ikiwa na meli zake za uvivi katika Bahari ya Hindi, wananchi upande wa visiwani Zanzibar kunufaika na uwepo wa zao la mwani, upotevu wa mazao ya samaki kupungua, uwepo wa mbegu bora za mahindi, alzeti na mimea mingine ya jamii ya kunde pamoja na kuanzishwa kwa viwanda vya kutengeneza chakula cha samaki, hatua itakayowezesha uwepo wa vifaranga vya samaki vyenye ubora.



