Dodoma tayari kwa mabalozi, serikali yatoa viwanja bure

JUMUIYA ya wanadiplomasia nchini imetakiwa kufi kisha taarifa katika serikali za nchi zao kuwa Dodoma ipo tayari na kuwa zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi ya balozi kwenye viwanja vilivyotolewa bure na Serikali ya Tanzania.

Serikali ya Tanzania ilitoa viwanja bure kwenye mji wa serikali, Mtumba jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo kwenye Mkutano maalumu wa Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini ulioandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Aidha, Kombo aliwaeleza mabalozi hao kuwa siri kubwa ya mafanikio yoyote duniani ni kuwa na imani na jambo unalolidhamiria kulitekeleza.

Alisema Serikali ya Tanzania tangu ilipofanya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi jijini Dodoma mwaka 1973 ilikuwa na imani na uamuzi huo na leo imani hiyo inatekelezwa kivitendo kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo ya miundombinu na huduma za kijamii ili kuuweka mji wa Dodoma katika mazingira mazuri ya kuishi, kwa watu wa aina yote, wakiwemo mabalozi.

Alisema kutokana na ujenzi wa mji wa Dodoma, fursa nyingi za uwekezaji zimeibuliwa, hivyo ametoa wito kwa mabalozi kuwaleta wawekezaji jijini Dodoma kuchangamkia fursa hizo.

Alitoa wito pia kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoa taarifa ya kila hatua ya ujenzi wa mji huo kwa wadau kwa lengo la kuhamasisha kufanya uamuzi sahihi kuhusu Dodoma.

Alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kupeana taarifa kuhusu maendeleo ya Mkoa wa Dodoma na
kupendekeza uwe unafanyika kila mwaka.

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

Mwenyeji wa Mkutano huo uliobeba kaulimbiu ‘Dodoma Ipo Tayari: Ipeleke Dodoma Duniani na Ilete Dunia Dodoma’, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alieleza hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa mji huo, hususani katika maeneo ya miundombinu ya huduma za afya, elimu, maji, umeme, usalama, usafiri na burudani.

Alisema huduma hizo zinapatikana kwa ubora wa kimataifa, hivyo jumuiya ya wanadiplomasia isihofie chochote inakaribishwa Dodoma na ipo tayari kwa ajili yao.

Alisema serikali ipo katika mchakato wa kujenga Mji wa Hombolo na kubainisha kuwa hiyo ni fursa kubwa na adhimu kwa wawekezaji kushirikiana na serikali kufanikisha ujenzi wa mji huo.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Kiongozi wa Mabalozi ambaye alikuwa Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga alisema yeye na mabalozi wenzake wameshuhudia hatua kubwa iliyopigwa katika ujenzi wa mji wa Dodoma hasa baada ya kutembelea na kujionea mji wa serikali uliopo eneo la Mtumba, Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa na ujenzi wa Kiwanja cha Ndegecha Kimataifa cha Msalato.

Alisema wameridhika na hatua iliyofikiwa na wameahidi kuzishawishi serikali za nchi zao kutenga fedha za kuanza ujenzi wa ofisi na makazi ya balozi jijini Dodoma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button