Mvutano wa Kariakoo Derby wazua mabadiliko makubwa TPLB

DAR ES SALAAM — Katika kile kinachoonekana kuwa ni matokeo ya mvutano mkali kuhusu upangaji wa mechi ya Kariakoo Derby, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza mabadiliko makubwa ndani ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, imethibitishwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto, amejiuzulu nafasi yake kufuatia mvutano wa muda mrefu kuhusu upangaji wa mchezo namba 184 wa Ligi Kuu unaozikutanisha klabu kongwe za Simba na Yanga.

Aidha, Rais wa TFF, Wallace Karia, amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo, ikiwa ni hatua nyingine ya kusafisha mazingira kufuatia sintofahamu iliyozunguka ratiba ya mchezo huo maarufu zaidi katika kalenda ya soka la Tanzania.

Mvutano ulianza baada ya klabu ya Yanga kupinga mabadiliko ya tarehe ya awali ya mchezo huo, ambao ulikuwa umepangwa kuchezwa Machi 8, kabla ya kuahirishwa ghafla bila maelezo ya kina. Hali hiyo iliibua hisia kali kwa mashabiki na wadau wa soka nchini, huku Yanga ikieleza wazi kutokuwa na imani na baadhi ya viongozi wa TPLB.

Baada ya hali kuendelea kuwa tete, mchezo huo ulipangwa kufanyika tena Juni 15, lakini ukasogezwa mbele tena hadi Juni 25, jambo lililoibua taharuki zaidi miongoni mwa mashabiki na vyombo vya habari.

Kriketi wanawake watinga nusu fainali Kwibuka

Arusha mguu sawa UMISSETA Taifa

Hatua ya kujiuzulu kwa Mguto na kusimamishwa kwa Kasongo inaashiria dhamira ya TFF ya kurejesha imani kwa wadau wa soka nchini na kuhakikisha uwazi na weledi katika upangaji wa ratiba ya ligi, hasa kwa michezo mikubwa kama Kariakoo Derby.

Kwa sasa, macho na masikio ya mashabiki wa soka yameelekezwa kwenye mchezo huo wa kiporo uliopangwa kuchezwa Juni 25, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button