Maji Ziwa Victoria kufikishwa Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema katika miaka mitano ijayo serikali yake itajenga mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma.

Ilani ya uchaguzi ya CCM 2025-2030 inasema mradi huo utapitia Singida na utakuwa na mabomba mawili.

Imeeleza bomba moja litakuwa la maji ya kunywa na lingine kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na mifugo.

Pia, CCM imeeleza katika miaka mitano serikali yake itaanzisha na kutekeleza Gridi ya Taifa ya Maji itakayotumia vyanzo vikubwa vya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, uchumi na mazingira.

Imetaja vyanzo hivyo ni Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

Katika Ilani CCM imeleeza inatambua umuhimu wa maji katika maisha ya kila siku ya wananchi, matumizi ya viwandani na kuimarisha hali ya usafi wa mazingira.

Aidha, chama hicho kimeeleza kinatambua kazi kubwa ambayo serikali imefanya katika miaka mitano iliyopita katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi hususani vijijini.

CCM imeeleza katika miaka mitano ijayo, serikali itakamilisha ujenzi wa mabwawa ya kimkakati ikiwa ni pamoja na bwawa la Kidunda na Farkwa ili kuongeza usalama wa maji nchini.

Imeeleza kwamba itaimarisha mifumo ya uondoaji wa majitaka nchini ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 13 hadi asilimia 40.

Ilani imeeleza chama hicho kitaongeza kasi ya uvunaji wa maji ya mvua kwa kujenga mabwawa ya ukubwa wa kati na mabwawa ya kimkakati kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kilimo, mifugo na uvuvi.

Chama hicho kimeeleza kwamba serikali yake itaongeza idadi ya kaya vijijini na mijini zilizofikiwa na huduma ya maji safi na salama kwa asilimia isiyopupungua 90.

Pia, ilani imeleeza serikali itajenga miradi ya maji na mitambo ya kutibu maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu ili kuimarisha usalama wa maji na itaimarisha ulinzi na uendelezaji wa vyanzo na rasilimali za maji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button