Maliasili yapongezwa kutekeleza maono ya Rais Samia

WIZARA ya  Maliasili na Utalii imepongezwa kwa kutekeleza kikamilifu maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Wizara ya kwanza kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi na kuwezesha Idara na Vitengo vyake kuhamia Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi ametoa pongezi hizo alipotembelea Wizara hiyo kwa lengo la kukagua ujenzi wa Majengo ya Serikali ambao ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia ya Serikali kuhamia Dodoma.

Lukuvi amesema Wizara ya Maliasili na Utalii licha ya kukamilisha mapema ujenzi wa jengo hilo, inastahili pia kupongezwa kuwa ya kwanza kuhamia na kuwa mfano katika matumizi ya samani za ofisini zilizozalishwa hapa nchini kupitia mazao ya misitu.

“Ninyi ni mabalozi wazuri wa matumizi ya bidhaa zetu za hapa nchini zinazotokana na misitu yetu, ni imani yangu kuwa Wizara zote zitaiga mfano huu,” ameongeza Lukuvi.

Aidha Lukuvi ametoa rai kwa watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha wanatunza vyema miundombinu na vifaa vilivyopo ili viweze kudumu kama ilivyokusudiwa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Hassan Abbasi amemshukuru Waziri Lukuvi kwa ziara yake, na kuahidi kuwa Wizara itatekeleza vyema maelekezo aliyoyatoa hususani ya usimamizi mzuri wa matumizi ya jengo na vifaa vilivyopo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button