Mbio nishati safi zaiva Arusha

ARUSHA: MKUU wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amewaaalika wananchi mbalimbali kujitokeza kushiriki mbio za riadha za Nishati Safi ya Kupikia zilizopangwa kufanyika Agosti 3 Njiro.
Akizungumza jana, RC Kihongosi alisema katika kuelekea Sikukuu ya Nanenane kutakuwa na mbio ambazo zitahusisha km 21, km 10 na km 5.
“Pia kuanzia Agosti 2 hadi 8 kutakuwa na mabanda ya teknolojia ya nishati safi ambayo yatafanyika eneo la Nanenane Njiro na kuwahisi wananchi wote wa mikoa ya jirani ikiwemo Manyara na Kilimanjaro na Arusha yenyewe kuja kushiriki.
Alieleza kuwa pia kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya nishati safi na elimu itatolewa kuhusiana na madhara ya kutumia nishati isiyosafi
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Business Women Association (TABWA) ambao ndio waandaaji, Noreen Mawalla amesema mbio hizo za kihistoria ni kuhamasisisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya mwanamke na Taifa kwa ujumla ambapo ni msimu kwanza toleo la pili na tayari zimefanyika jijini Dar es salaam , ambapo watu 436 walishiriki.
“Tukio hili linafanyika kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Nishati Safi ya Kupikia, inayolenga kuhakikisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2032.
Aidha, juhudi hizi ni mwitikio wa wito wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa mapambano ya kuondoa matumizi ya kuni na mkaa barani Afrika, kupitia kaulimbiu yake maarufu: “Tumtue Mama Kuni Kichwani.” amesema Mawalla.
Alisema Clean Cooking Marathon ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika katika kanda zote 5 za Tanzania, ikilenga kuelimisha jamii juu ya athari za matumizi ya nishati chafu, kuongeza ufahamu kuhusu nishati mbadala, na kushirikisha wadau mbalimbali katika kuharakisha na kuchochea mabadiliko chanya.
“Kauli mbiu ni Nishati safi ya kupikia,Linda Afya ,hifadhi mazingira kwa uchumi endelevu na tunatoa wito kwa wananchi wote, mashirika, na sekta binafsi kushiriki kwa wingi kuelekea kilele cha mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Agasti 3 mwaka huu eneo la Njiro, Arusha,”ameongeza Mawalla.



